NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania ,Sheikh Ponda Issa Ponda amejiunga rasmi, Chama cha Act Wazalendo huku akipewa rasmi kadi ya heshima ya Maalim Seif pamoja na Katiba ya Chama hicho ikiwa kama nyenzo katika shughuli zake za kisiasa ndani ya chama hicho.
Mapokezi hayo ya kumkaribisha Sheikh Ponda yameongozwa na Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Chama hicho pamoja na Ngome zake katika makao makuu ya Chama hicho Magomeni Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kabla ya kumkabidhi Sheikh Ponda kadi na Katiba ya Chama hicho,Kiongozi wa Chama cha Act Wazalendo,Dorothy Semu amesema ana imani kubwa na Sheikh Ponda kuingia katika Chama hicho kwani ataweza kusaidia kuongeza nguvu kwenye kampeni yao ya kupigania haki na kutetea Demokrasia.
Amesema ACT Wazalendo ina kampeni mahsusi wanayoendeleza Operesheni linda haki na Demokrasia, hivyo anawakaribisha wapenzi wote wa Demokrasia kujiunga na chama cha ACT Wazalendo.
Semu amesema wajibu wao kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni kutoa Jukwaa la Mapambano ambalo linaing’oa,Chama cha Mapinduzi CCM wanahakika wakiendeleza mapambano hayo watashinda uchaguzi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
”Leo ni siku ya Sheikh Ponda tumesikia miaka mingi sana,Sheikh Ponda Issa Ponda ni mwamba wa harakati,ninafuraha kwaniaba ya Chama kumpokea ili aendelee na harakati zake kupigania haki akiwa ndani ya Act Wazalendo.
”Tunakushukuru Sheikh Ponda kwa heshima kubwa uliyokipa Chama chetu,tumesikia historia yako imeturudisha nyuma kufikiria harakati za mapambano kutafuta haki na usawa katika nchi,”amesema.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho,Ado Shaibu amesema amefurahi ujio wa Sheikh Ponda katika Chama chao kwani kila jambo na wakati wake.
Amesema historia ya chama chao ipo kama ilivyokuwa ya vyama vingine wamepitia nyakati nyingi za furaha na huzuni pamoja na mapambano makali na mepesi.
”Leo ni siku ya Issa POnda tunamfahamu kwa mengi uwanja wa siasa jina lake sio geni,zipo nyakati alipanda katika majukwaa mbalimbali kama CUF,CHADEMA lakini hakuwa na kadi ya uanachama katika vyama hivyo.
”Ila leo Sheikh Issa kaamua kuchukua kadi Act Wazalendo,Sheikh Ponda hapaswi kuelezewa anajipambanua yeye mwenyewe na historia yake ya kutetea haki za binadamu,”amesema.
Naye Sheikh Ponda amesema malengo yake makubwa yakuchukua kadi ya Chama ch Siasa ni kujiimarisha kisheria ili kupata jukwaa la kuwaelimisha wananchi kujua ajenda kuu ya taifa lao na kuwahamasisha kupigania mambo ya msingi.
”Nimeona umuhimu wa kuchangia nguvu katika Operation ya Act Wazalendo ya Linda Demokrasia inayolenga kurejesha haki ,uwazi na usawa katika mchakato wa uchaguzi nchini,”amesema
Amesema mapambano ya kudai haki sio ya mtu mmoja wala chama kimoja bali yanahitaji umoja wa wapigania haki wote ikiwemo wale walioko katika vyama vya iasa ,viongozi wa dini na kila mtanzania anaejali musktakabali wa taifa.
Aidha amesema ni umuhimu viongozi wa dini kushiriki siasa kwani uwepo wao katika vyombo vya maamuzi ni muhimu sana,utasaidia kulinda maadili ya utu na taifa.