NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA) imetoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya Dk.Samia Suluhu Hassan Madarakani.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo Vya Habari jijini Dar Es Salaam leo Aprili 14,2025 Mkurugenzi Mkuu wa LATRA Habibu Suluo amesema Mamlaka miongoni mwa mafanikio makubwa ni udhibiti Usafiri wa Barabara na Utoaji Leseni kwa Vyombo vya Usafiri kwa Njia ya Barabara
Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)( b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, LATRA ina wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na/au kufuta leseni za usafirishaji. Idadi ya leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria (passenger service vehicles), mizigo (goods carrying vehicles), na vyombo vya usafiri wa kukodi (private hire service vehicles) ziliongezeka kutoka 226,201 mwaka 2020/21 (Februari, 2021) hadi 334,859 mwaka 2024/25 (Machi, 2025), ikiwa ni ongezeko la leseni 108,658, sawa na ongezeko la asilimia 48. Hili ongezeko ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne (4).
Amesema kuwa,LATRA imefungua ofisi ndogo kumi (10) kwenye maeneo mbalimbali ya kimkakati na hivyo kuwa na jumla ya Ofisi 37 nchi nzima. Kufikia mwezi Machi 2025, ofisi hizi ndogo zimeonesha mafanikio katika kufikia wananchi walio mbali na miji mikuu ya mikoa, kuboresha udhibiti wa bodaboda, kutatua migogoro ya wadau katika maeneo hayo, kufikisha elimu kwa wadau na kusogeza ushirikiano na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo hayo, ikiwemo Serikali za Mitaa (LGAs), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na mamlaka zingine zilizopo kwenye maeneo hayo.
Aidha Suluo amesema LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika miji na majiji makubwa hapa nchini. LATRA imeanzisha njia mpya 1,007 za daladala Mkoani Dar es Salaam ili kufika maeneo yasiyofikika na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kumpunguzia gharama mwananchi.
Akieleza Njia za usafiri wa mabasi ya mijini zilizorefushwa Suluo alizitaja kuwa ni Dar es Salaam
i) Mbezi Luis – Kisarawe kupitia barabara ya Malamba Mawili, Banana ii) Toangoma – Pugu Stesheni kupitia barabara ya Kilwa, Nyerere iii) Kivukoni – Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo, iv) Gerezani – Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo,
v) Buyuni Sokoni – Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Kinyerezi vi) Bunju Sokoni – Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Madale
vii) Mbande Kisewe – Gerezani kupitia Barabara ya Kilungule, Chang’ombe,
Usalama, viii)Mvuti – Machinga Complex na Tabata Segerea, ix) Ngobedi B -Machinga Complex kupitia Nyota Njema, na x) Kitonga – Gerezani kupitia barabara ya Kilwa.
Suluo anebainisha kuwa mafanikio mengine ni LATRA kufanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya baadhi ya njia kuwa za mzunguko kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na huduma. Mfano ni njia inayoanzia Kwa Mrombo kupitia Impala, Philips, Sanawari, Chuo cha Ufundi Arusha hadi ‘Fire’ na kurudi kwa Mrombo.
Amesema kuwa,katika Jiji la Dodoma, Makao Makuu ya nchi, zimeanzishwa njia mpya kwa ajili ya kuyafikia maeneo mapya ya makazi mapya kutokana na kukua kwa kasi kwa Jiji la Dodoma. Mfano wa njia hizo ni:
i) Machinga Complex – Njedengwa, ii) Machinga Complex – Mpamaa, iii) Machinga Complex – Chidachi, iv) Machinga Complex – Nzuguni,
v) Machinga Complex – Swaswa, na vi) Vyeyula – Ilazo.
Hatua ya kuhamishia daladala kituo cha Machinga Complex kumesaidia kuwepo kwa njia za mzunguko katikati ya Jiji la Dodoma na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Mzunguko huo ni kuanzia barabara ya Hospitali kupitia Majengo Sokoni hadi Machinga Complex kisha kupitia Uwanja wa Ndege na kurudi mjini.
Katika Jiji la Mwanza Suluo amesema, zimeanzishwa njia ndefu kwa ajili ya kuyafikia maeneo mapya ya makazi na kukua kwa kasi kwa Jiji la Mwanza. Mfano wa njia hizo ni kutoka:
i) Usagara – Kisesa kupitia Buzuruga; ii) Ilalila – Misungwi kupitia Buzuruga; iii) Nyashishi – TX kupitia Kiseke – PPF; iv) Nyashishi – Kisesa Kona ya Kayenze kupitia Mecco v) Nyashishi – Ilalila kupitia Buzuruga; vi) Mwanza mjini – Igombe vii) Mwaloni – Kona ya Kayenze; na viii) Mwaloni – Kabusungu.
Kwa upande wa Uthibitishaji wa Madereva Suluo ameainisha kuwa
Kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya LATRA Sura 413, LATRA ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafirishji vinavyodhibitiwa. Lengo la kuthibitisha madereva ni kuwa na madereva wenye weledi wa kuendesha magari yanayotoa huduma za usafiri wa umma na mizigo kwa usalama.
“Mamlaka imekuwa ikiwasajili madereva na baadae kuwapatia vyeti vya kuthibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa inayofanyika katika Ofisi za LATRA za Mikoa yote 26 Tanzania Bara.
” Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2025, madereva 33,778 walikuwa wamesajiliwa na taarifa zao kuingizwa kwenye Kanzidata (Database) ya Mamlaka. Kati ya madereva hawa, madereva 8,172 wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) na kupatiwa Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i-button), na madereva 4,563 walifaulu mitihani ya LATRA kati ya 9,191 waliofanya mitihani huo (sawa na ufaulu wa asilimia 49.65) na kupatiwa vyeti vya kuthibitishwa.
” Matokeo haya yanaashiria maandalizi hafifu kwa madereva, woga wa mitihani unaofanywa kwa kompyuta, upya wa zoezi la kuthibitisha madereva, na kukosekana kwa utaratibu wa kujisomea/kujiendeleza kwa madereva. “amebainisha Suluo
Wakati huo huo Suluo amejinasibu kuwa, tangu kuanza kwa huduma za usafiri wa 24/7, LATRA imeendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani katika uratibu wa huduma za usafiri wa mabasi kwa kuimarisha usimamizi wa masharti ya leseni ikiwemo ukaguzi wa mabasi, utambuzi wa madereva kwa i-buttons na kongeza matumizi ya VTS. Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2025, mabasi 2,323 yalikuwa yamepatiwa ratiba za kutoa huduma za usafiri usiku na mchana (24/7).
Aidha, tathmini ya LATRA ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa ruhusa hii ya safari za usiku na mchana (24/7) umeonesha Wananchi wengi wamefurahishwa na kuridhishwa na maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dk.Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mabasi kusafiri usiku.
Suluo ameeleza kuwa kuna mwitikio mkubwa wa Wananchi kutumia usafiri wa usiku kuliko mchana, na msongamano wa abiria kwenye Stendi umepungua sana, na ‘mchezo’ wa mabasi kukimbizana umepungua sana na unaelekea kwisha kabisa. Vilevile, tathmini ya LATRA inaonesha kuwa safari hizi za 24/7 zimepunguza gharama za njiani kwa abiria na kuboresha matumizi ya muda wao kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na kujiongezea vipato.
Kuhusu Udhibiti wa Usalama wa Huduma za Reli ,Suluo amesema, Usafirishaji kwa njia ya reli nchini ni mojawapo ya eneo linalodhibitiwa na LATRA kwenye maeneo ya usalama wa miundombinu na mabehewa, nauli, viwango vya ubora na ufanisi wa utendaji. Katika hatua ya kutimiza majukumu haya, LATRA katika kipindi kinachoanzia Februari, 2021 hadi Machi, 2025 imefanya jumla ya kaguzi 275 katika miundombinu, ishara na mawasiliano, vitembea reli (vichwa na mabehewa) na uendeshaji. Kati ya kaguzi hizi, 143 zilikuwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), na kaguzi 132 zilikuwa kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Katika hatua nyingine Suluo ameeleza kuwa Uanzishwaji wa Huduma za Treni za SGR , LATRA ilikuwa na jukumu la kuthibitisha ubora wa vitembeareli kabla ya kuanza kutoa huduma. LATRA iliungana na timu ya wataalamu wa TRC na Wizara ya Uchukuzi kwenda Nje ya Nchi (zilikokuwa zinaundwa) na kukagua na kuthibitisha. Jumla ya vichwa vya treni 17, Mabehewa ya abiria 56, treni za seti za umeme (EMU) 10 na Mabehewa ya mizigo 264 yamekaguliwa kipindi cha uundwaji katika nchi za Korea, China, Malaysia na Ujerumani. Pia Mamlaka imefanya kaguzi za majaribio kwa mabehewa na vichwa hivyo baada ya kuwasili nchini kabla ya kuanza kutumika kutoa huduma.
Katika mwaka wa fedha 2023/2024, LATRA ilitekeleza jukumu la kisheria chini ya Kifungu cha 5(1)(c) kwa kupanga nauli za daraja la uchumi (Economy Class) wakati wa uanzishwaji wa huduma za treni ya kisasa (SGR). Kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya LATRA, Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA iliidhinisha nauli za abiria kwa daraja la uchumi (economy class) kwa treni inayosimama kila kituo na treni inayosimama vituo maalum (express train) na kuanza kutumika mwezi Juni 2024.
Nauli za Treni ya SGR zilitangazwa kwa Taarifa ya Kawaida Na 8931 kwenye Gazeti la Serikali Toleo Na 24 la 14 Juni 2024 zikiwa ni Shilingi 31,000 kwa treni ya kawaida (inayosimama kila kituo) na Shilingi 50,000 kwa treni inayosimama vituo maalum (express) kati ya Dar-es-Salaam na Dodoma. Nauli zilizoidhinishwa zimeelekeza mtoto mwenye umri kuanzia miaka minne hadi miaka 12 kutozwa nusu ya nauli na mtoto mwenye umri chini ya miaka minne kutotozwa nauli. Aidha, LATRA iliruhusu TRC kujipangia nauli za SGR kwa Daraja la Biashara (Business Class) na madaraja mengine ya juu (Royal Class) kwa kuwa eneo hili ni kwa abiria wenye uwezo kifedha na wanaoweza kufikia huduma hii.
Akielezea Udhibiti Usafiri wa Waya (Cable Transport Regulation) Suluo amesema, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa (2021/2022 hadi 2025/2026) imeelekeza maboresho katika huduma za utalii nchini. Katika kutekeleza jukumu hili, LATRA imefanya utambuzi wa mahitaji, utayari wa wadau, na maeneo ya uwekezaji nchini. Tathmini ya awali ya LATRA imebainisha maeneo yenye vivutio yaliyopo kwenye mikoa nane (08) ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, na Mbeya. Aidha, rasimu ya Kanuni za Udhibiti wa Usafiri wa Waya zilishaandaliwa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikisha wadau.
” Kanuni hizo zilijadiliwa kwenye kikao cha Wadau kilichofanyika tarehe 23 Disemba 2024. Pia, Bodi ya LATRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara ya Uchukuzi, na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inakamilisha mapitio ya Muundo wa Uongozi na Mgawanyo wa Majukumu ili kuunda Kitengo cha Udhibiti Usafiri wa Waya na kuwezesha usimamizi wa Kanuni za Usafiri wa waya, pindi zitakapokamilika na kuidhinishwa na Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 45 ya Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413. ”
Kuhusu Udhibiti Usafiri wa Reli ,Suluo amesema Latra imefanikiwa
Udhibiti wa Usalama wa Huduma za Reli
ambapo Usafirishaji kwa njia ya reli nchini ni mojawapo ya eneo linalodhibitiwa na LATRA kwenye maeneo ya usalama wa miundombinu na mabehewa, nauli, viwango vya ubora na ufanisi wa utendaji. Katika hatua ya kutimiza majukumu haya, LATRA katika kipindi kinachoanzia Februari, 2021 hadi Machi, 2025 imefanya jumla ya kaguzi 275 katika miundombunu, ishara na mawasiliano, vitembea reli (vichwa na mabehewa) na uendeshaji. Kati ya kaguzi hizi, 143 zilikuwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), na kaguzi 132 zilikuwa kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Pamoja na mambo yote ,Suluo ametoa Shukrani kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia uzima, na fursa ya kukutana kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu mafanikio ya utendaji wa LATRA katika kipindi cha miaka minne (4) ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dk.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“,Napenda kutumia fursa hii kutoa Pongezi za Dhati kwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Uongozi wake mahiri wa Serikali ya awamu ya sita wenye mafanikio mengi makubwa. Kwa maneno uchache, niseme tu kwamba, Uongozi wa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan umetujengea mazingira rafiki yenye ushirikishaji wa wadau katika kusimamia sekta ya usafiri ardhini.
” Ninawapongeza pia uongozi mahiri na madhubuti wa wasaidizi wake, wakiwemo Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Prof. Godius W. Kahyarara, Katibu Mkuu – Wizara ya Uchukuzi, pamoja na Mha. Ludovick Nduhiye, Naibu Katibu Mkuu – Wizara ya Uchukuzi.
,”Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana watoa huduma zinazodhibitiwa na LATRA, watumiaji wa huduma za usafiri ardhini, pamoja na wadau wetu wote, zikiwemo taasisi za umma na sekta binafsi kwa ushirikiano waliotupatia katika katika kipindi chote cha utendaji wetu. LATRA imepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wetu mmoja mmoja na kupitia vyama vyao ikijumuisha TABOA, TAT, TATOA”