NA MWANDISHI WETU ,DAR ES SALAAM
KATIKA kuadhimisha siku ya wanawake duniani yenye kauli mbiu inayosema “Wanawake na wasichana 2025: Tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji”, Wakala wa Vipimo (WMA) imetoa wito kwa wanawake kutumia vipimo vilivyo sahihi katika biashara na shughuli zao za kilasiku.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mkuu wa Kitendo cha Tehama Wakala wa Vipimo (WMA), Rose Juma amesema wao kama WMA wanatumia maadhimisho hayo kutoa elimu kwa wanawake juu ya matumizi sahihi ya vipimo.
Amesema kama watu wanavyojua wanawake ni walezi katika jamii na ndio watumiaji wakubwa wa vipimo hivyo wataendelea kutoa elimu juu ya utumiaji wa vitu hivyo kwa usahihi hasa katika biashara na shughuli zao.
“Kama tunavyojua wanawake ni walezi katika jamii na tunaamini pia ni watumiaji wakubwa wa vipimo hivyo tunataka waendelee kutumia kwa sahihi na pale wanapodhani vipimo vinavyotumika havipo sahihi wanashauriwa kutoa taarifa WMA, tuna ofisi nchi nzima katika kila mkoa, toeni taarifa ili tuweze kufanyia kazi. Ninawatakiwa wanawake wote heri ya siku ya wanawake duniani ya mwaka 2025” amesema