NA ATUPAKISYE MWAISAKA, DAR ES SALAAM
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),imezifutia usajili Kampuni 11 ambazo zimekiuka masharti ya Kifungu cha 400A (1) (e) cha Sheria ya Kampuni Sura 212 kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za kampuni hizo na miongozo ya uendeshaji wa kampuni wakati wa usajili.
Kampuni hizo ni pamoja na LBL Mtwara Media Company Limited (Na. 181289972), LBL Morogoro Media Company Limite1d (Na. 179770873), LBL Geita Advertising Media Limited (Na. 180439242), LBL Mbeya Media Limited (Na. 179978326),LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited (Na. 181302259),
Nyingine ni LBL Mbezi Advertising Media Company Limited (Na. 180582835),LBL Ubungo Media Limited (Na. 180960333),LBL Mabibo Media Company Limited (Na. 181117346),LBL Mbagala Media Company Limited (Na. 181248874) ,LBL Gongo la Mboto Media Advertising Company Limited (Na. 181513438) na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Company Limited (Na. 180046992).
Akizungumza hayo Leo Machi 5,2025 jijini Dar es Salaam,Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA , Goefrey Nyaisa wakati akiongea na Waandishi wa Habari amesema kutokana na kukiukwa kwa Kifungu hicho, sheria inamtaka Msajili kuchukua hatua chini ya Kifungu hicho 400A (1) (e) ambazo ni kuijulisha kampuni kuhusu ukiukwaji na hatua anazokusudia kuzichukua kwa kampuni husika.
“Sheria inaendelea kueleza kuwa, endapo kampuni itashindwa kutoa maelezo, au kutoa maelezo yasiyoridhisha, Msajili atafuta kampuni husika kwenye Rejista ya Kampuni,hivyo kwa mujibu wa Kifungu hicho msajli alizijulisha kampuni husika kuhusu kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya Januari 2 na 26,2025, na kwa kuwa kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu 400A (2), Msajili amezifuta rasmi kampuni kwenye Rejista ya Kampuni kuanzia Februari 27,2025,”amesema
Aidha Nyaisa amesema hakuna sheria wala taasisi yenye mamlaka ya kutoa vibali wala leseni za kufanya biashara za upatu hapa nchini.
” Msajili anaendelea na ufuatiliaji wa kampuni nyingine zinazofanya shughuli za kibiashara nje ya katiba zao na kinyume na Sheria na taratibu huku kuzichukulia hatua stahiki ikiwemo kuzifuta kwenye Rejista ya Kampuni.
Nyaisa ameeleza kuwa biashara ya upatu ni kinyume na sheria za nchi na hivyo wananchi wanahimizwa kutoa taarifa mara moja kwa Mamlaka husika, zikiwemo taasisi za Kiserikali na Jeshi la Polisi, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya kampuni au watu wanaofanya au kujihusisha na biashara hiyo.