NA MWANDISHI WETU,MOROGORO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Hamad Masauni amesema kituo cha Taifa cha ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) nchini kilichopo katika Chuo Kikuu Cha Sokoine
Cha Kilimo (SUA)mkoani Morogoro kitakuwa ni miongoni mwa taasisi muhimu nchini katika kusaidia Taifa kutokana na miradi mbalimbali ambayo mataifa ya nje yanakuja kuwekeza kupitia biashara ya Kaboni, ili biashara hiyo iweze kusaidia katika kukuza kipato cha wananchi lakini pia kuchangia uchumi wa nchi kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo Februari 8,2025 alipofanya ziara ya kutembelea kituo hicho kilichopo mkoani Morogoro.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima katika ziara hiyo amesema mkoa huo umejipanga kutumia vyema fursa hiyo ili kutekeleza na kutafsiri kwa vitendo maelekezo na maono ya Rais Samia ya kuhakikisha biashara ya Kaboni inakuwa vyenzo vyengine ya kuinua kipato cha wananchi na kuchangia katika maendeleo nchini.
“Ni fursa muhimu sana kwetu uwepo wa kituo hiki mkoani kwetu ni hatua muhimu sana, kwani vianzio vyote vinavyopelekea biashara hii kufanyika tunavyo kupitia misitu, mifugo na mito tutahakikisha fursa hii inatumika vyema na tija iweze kuonekana kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kupitia rasilimali tulizonazo” alisema Shaka.