NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAKUU wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wametoa maazimio 22 yanayolenga kumaliza mgogoro uliyopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Maazimio hayo yametoka baada ya Wakuu hao kujadiliana kwa takribani zaidi ya saa sita Ikulu jijini Dar es Salaam leo Februari 8,2025 na kusomwa na Katibu Mkuu wa SADC, Veronica Muen Nduva mbele ya Waandishi wa Habari.
Akisoma maazimio hayo, Katibu Nduva amesema kwa pamoja viongozi hao wameazimia kuagiza Wakuu wa Majeshi wa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kukutana ndani ya siku tano na kuchukua hatua za kusitisha mapigano bila masharti.
Amesema pia Wakuu hao wameazimia kuandaa mpango wa usalama kwa mji wa Goma, kuruhusu wananchi waliopo katika mji huo watibiwe na kupatiwa misaada ya kibinadamu pamoja na kufungua uwanja wa ndege wa mji wa Goma.
Sambamba na hilo, wakuu hao wameazimia kwa pamoja na kuwataka Mawaziri wa nchi za EAC/SADC kukutana ndani ya siku 30 kujadili na kutoa mrejesho wa kile kilichoamuliwa na wakuu wa majeshi kuhusu kusitisha mapigano DRC-Congo.
Nduva amesema mengine yaliyoazimiwa katika kikao hicho ni pande husika za mgogoro huo kufanya mazungumzo ya moja kwa moja, ambayo yatahusisha pia wanajeshi na wasio wanajeshi, ikiwa ni pamoja na Kundi la M23 na mengine ni kuondolewa kwa vikosi vya kigeni visivyoalikwa ndani ya DRC.
“Wakuu hao wa nchi wamethibitisha kuendeleza mshikamano na kujitolea kuendelea kuiunga mkono DRC na kuhakikisha inapata uhuru wa eneo lake.
“Kuwepo kwa majadiliano kama haya mara moja kila mwaka ili kufanya tathmini ya mzozo huo na kuwaalika viongozi wa Afrika Mashariki kila mwaka kupitia masuala hayo ya DRC”amesema
Aidha Wakuu wa nchi hizo walimpongeza Rais William Ruto, Mwenyekiti wa EAC kwa kuitisha na kuongoza majadiliano hayo huku wakimpongeza Dk. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo.