NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
KIONGOZI wa Chama cha ACT –Wazalendo, Dorothy Semu ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari na Wahariri leo Januari 16, 2025, Dorothy amesema yupo tayari kumkabili Rais Samia Suluhu Hassan wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwamba hatua hiyo imesukumwa na mambo kadhaa ambayo ameyaona kama mapungufu.
Amesema yupo tayari kumkabiri Rais Samia endapo chama chake kitampatia ridhaa hiyo na kwamba amejipima na ameona anatosha kuwa kiongozi kwenye nafasi hiyo.
“Mimi ni kiongozi wa chama bora, chenye sera na ilani bora, nimejipima na nimeona natosha kuwania nafasi hii ya uraisi ,” amesema Semu.
Aidha Semu ameyataja baadhi ya mambo yaliyoyaona yanamapungufu kuwa ni kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, kupanda kwa gharama za maisha, changamoto ya ajira kwa vijana na udhaifu katika usimamizi wa rasilimali za Taifa.