*YUMO PIA KINARA WA DAWA ZA KULEVYA JIJINI DODOMA
NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata Kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya, Milimita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya huku watuhumiwa 58 wakikamatwa.
Dawa hizo zimekamatwa katika oparesheni iliyofanywa na mamlaka hiyo kwenye maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 12,2024 Kamishna Jenerali DCEA, Aretas Lyimo amesema katika oparesheni hiyo jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi na lita 19,804 za kemikali bashirifu zimeteketezwa.
Amesema kati ya dawa hizo za kulevya zilizokamatwa, kilogramu 687.3 ni za skanka na kilogramu moja ya hashishi zilizokamatwa eneo la Goba jijini Dar es Salaam zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
Aidha amesema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, mamlaka ilikamata milimita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi pamoja na milimita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi.
“Dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu zikiwa zimewekwa chapa bandia za dawa za kuogeshea Mbwa na Paka ili kuepuka kubainika,” amesema
Amesema kukamatwa kwa dawa hizo ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya na kwamba hali hiyo inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya hivyo kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya.
Kinara biashara dawa za kulevya Dodoma akamatwa
Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Lyimo amesema Wafanyabiashara wawili wa dawa za kulevya akiwemo kinara wa dawa hizo Suleiman Mbaruku Suleiman maarufu kwa jina la Nyanda mwenye miaka 52 na Kimwaga Lazaro (37) wamekamatwa na dawa za kulevya aina ya heroini zenye jumla ya gramu 393.
Lyimo amesema kinara huyo na mwenzake wote ni wakazi wa Dodoma mtaa wa Kinyali kata ya Viwandani.
Amesema mtuhumiwa Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara hiyo ya dawa za kulevya mkoani humo na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu.
“Nyanda tumekuwa tukimfatilia kwa muda mrefu hadi tulipomkamata, tumeendelea kufanya oparesheni nchi nzima kupitia ofisi zetu za kanda na tumefanikiwa kukamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema
Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya nia thabiti ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kuwa tatizo la dawa za kulevya linakomeshwa ili kulinda afya na usalama wa watanzania.
“DCEA tunawaomba wananchi waendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi ya dawa za kulevya, “ amesema