NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Mapinduzi, Zanzibar( SMZ) imefadhili wanafunzi 200 kujiunga na Chuo Cha Ufundi Furahika ambacho kipo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchukua mbalimbali zinazofundishwa chuoni hapo.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Dk David Msuya, watasoma kozi ushonaji, hoteli, ususi, upambaji, urembaji na nyinginezo kwa lengo la kuweza kujiajiri ama kuajiriwa pindi watakapohitimu mafunzo hayo.
Mkuu huyo wa Chuo hicho amebainisha leo, Novemba 11, 2024 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari na kufafanua kuwa sasa Chuo hicho kina Wafunzi zaidi ya 400 wengine wakitokea Tanzania Bara wakiwa wanasoma kozi mbalimbali chuoni hapo.
“Kwa kipekee namshukuru sana na kumpongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Alli Mwinyi na Serikali yake kwa ujumla kwa kuthamini vijana waliotoka katika mazingira magumu na kuwaleta hapa ili wapate elimu itakayowezesha kujikwamua kichumi na kuachana na utegemezi kutoka kwa wazazi ama walezi wao,” amesema.
Ameongeza kwamba wanachotakiwa wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kutoingusha Serikali ambayo imejitolea kuwafadhili ili wafikie malengo yao katika elimu na kupatia ujuzi utakaowafaa maishani.
“Hizi fedha ambazo Rais Dk Mwinyi amezotoa kwa ajili ya kuwafadhili wanafunzi hawa zingeweza kwenda kufanya shughuli nyingine lakini amezitoa kwao ili waweze kujikwamua kielimu na kuweza kujitegemea, wanachotakiwa ni kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao ambazo zilionekana kuanza kupotea,” amesema.
Pia Dk Msuya hakusita kumpongeza Mkurugenzi wa Maendeleo ya jamii, Zanzibar kwa kuonesha ushirikiano na chuo hicho na kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na kujitegemea.
Toa
Mbali na hilo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kukiamini chuo hicho na kufungua milango kwa vijana ambao ndoto za kuendelea na elimu zilishatoweka ila kupitia chuo hicho wamepata tumaini jipya katika maisha yao.
Kwa upande mwingine, Dk.Msuya ametoa wito wa wazazi na walezi kupeleka vijana wao katika chuo hicho ili kupata ujuzi bure kupitia fani wazitakazo ikiwemo udereva, umeme na nyinginezo bure na tayari dirisha la usajili lipo wazi.
“Niwaombe wazazi na walezi pasipo kujali itikadi ya dini wala siasa wawalete watoto wapate ujuzi hapa elimu ni bure na tunakozi nyingi ambazo mtoto akitoka hapa ataweza kujiajili na kuajilika”,amesema.
Aidha ameongeza kuwa wameongeza kozi ya Tehama lakini pia wanatarajia kuanzisha kozi ya ufundi wa pikipiki ili kuhakikisha wanamgusa kila kijana ili waweze kujitegemea.
Mwanafunzi, Safia Hamis Mwinyi, kutoka Zanzibar, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi kwa kuwafadhiri na anaamini elimu hiyo itaenda kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuwaondoa kwenye utegemezi na kuweza kuwasaidia wazazi wao.