NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana amewataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan ambazo ni maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding).
Sambamba hilo Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kusimamia kwa mara nyingine Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ameyasema hayo leo Agosti 19,2024 aliporipoti katika ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, Mtumba jijini Dodoma alipozungumza na Watumishi.
Pia, ameitaka Menejimenti ya Wizara hiyo, kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.
“Muweke mikakati ya kukabiliana na changamoto hii, Mtanzania ni lazima tumlinde, muwe macho muda wote kutoa taarifa kwa wananchi na kukutana na Serikali za vijiji kuwaelimishe wasifike katika maeneo ya korido za wanyamapori ”amesema Chana
Waziri Chana ameongeza kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu na kuitaka menejimenti hiyo na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kukamilisha ahadi zote zilizoahidiwa kutekelezwa kipindi cha hotuba.