NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
KAMISHNA wa Uhifadhi, Mussa Kuji Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) leo Agosti 7,2024 amepokea jumla ya magari 13 yaliyofanyiwa matengenezo na Shirika la kimataifa linalojihusisha na Uhifadhi, Frankfurt Zoological Society (FZS) chini ya mradi wa Emmergency and Recovery Support for Biodiversity (ERSB).
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika ofisi za FZS, Arusha, Kamishna Kuji amesema “magari tuliyoyapata yataelekezwa katika shughuli za uhifadhi na utalii ili kuleta tija katika ulinzi wa maliasili zilizomo katika Hifadhi za Taifa“
Aidha, Kamishna Kuji alitoa wito kwa FZS kuendelea kuongeza wigo zaidi katika kuendeleza juhudi za uhifadhi ili kusaidia jamii kubwa ya watanzania.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Frunkfurt Zoological Society (FZS), Dk. Ezekiel Dembe ameeleza kuwa TANAPA inashirikiana vizuri na Shirika hilo katika kuendeleza uhifadhi na kwamba magari waliyoyatengeneza yatagawanywa katika Hifadhi za Taifa zaidi ya kumi (10) ili kuendeleza shughuli za uhifadhi.
Hifadhi za Taifa zitakazonufaika ni pamoja na Burigi-chato, Mto Ugalla, Ibanda-kyerwa, Kisiwa cha Rubondo, Milima ya Mahale, Rumanyika-Karagwe, Mkomazi, Serengeti, Ziwa Manyara na Katavi.
Magari hayo 13 yalichukukuliwa mwaka jana na FZS kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti yakiwa mabovu na kuanza kuyatengeneza kwa kutumia mafundi wa ndani.
Shirika la Frunkfurt Zoological Society (FZS) limekuwa na mchango mkubwa kwa kuonyesha jitihada katika uhifadhi wa maliasili hapa nchini ikiwemo kusaidia miradi mbalimbali inayojumuisha jamii na uhifadhi.