NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezitaka Mamlaka husika kuhakikisha wahusika wote watano wanaodaiwa kumbaka na kumlawiti msichana mmoja pamoja na aliyewatuma kufanya hivyo kukamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
LHRC imetoa kauli hiyo kufuatia kusambaa kwa video ikimuonesha msichana huyo kutoka Dar es Salaam, Wilaya ya Temeke, Kata ya Dovya akibakwa na kulawitiwa na vijana watano waliodai kuwa ni Askari wa moja ya vikosi vya ulinzi Tanzania.
Askari hao walimrekodi msichana huyo wakiwa wanamfanyia vitendo hivyo vya kikatili na kusambaza video hizo mitandaoni kwa maagizo ya kiongozi wao (Afande) ambaye aliwatuma kumpatia msichana huyo adhabu.
Kwa mujibu wa maelezo ya Askari hao, kosa la msichana huyo ni kutembea na mume wa bosi wao (Afande) ambapo katika mahojiano kwenye video tatu tofauti yanaonesha msichana huyo amekamatwa na kubakwa na kulawitiwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 5,2024, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga amesema Jeshi la Tanzania ni lenye heshima barani Afrika na duniani hivyo lihakikishe linajitenga na kashfa hiyo ya ubakaji wa raia wake kwani lina jukumu la kuwalinda (kama kweli wahusika ni wanajeshi).
Amesema vyombo vyote vya ulinzi na usalama viungane katika kuwatambua na kuwakamata wahusika na kama kweli ni wanajeshi wachukulie hatua za kijeshi na kiraia kuhakikisha haki inatendeka na imani ya jamii kwa jeshi inarudi.
“Tunamuomba rais wa Tanzania akiwa kama wanamama na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi kutoka hadharani na kuonyesha kuchukizwa na jambo hili la udhalilishaji na ukatili juu ya mtoto wa kike akiwa kama wazazi na kiongozi mwenye dhamana ya kulinda raia wa Tanzania.
“Tukifumbia macho mambo haya yatazidi kujitokeza zaidi katika jamii yetu kwa mwavuli wa watu kutumia nafasi zao kuumiza na kudhalilisha watu wengine,” ameesema Dk. Henga
Aidha amesema tukio hilo ni mwendelezo wa matukio mengi ya ukatili uliokithiri kwenye jamii ambayo LHRC kimekuwa kikikemea mara kwa mara.
“Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalinda heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa tu kwa wake na waume na kupinga ubaguzi wowote ule. Mkataba wa Kimataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya Wanawake wa 1979 unasisitiza kwamba ubaguzi dhidi ya wanawake unakiuka kanuni za usawa wa haki na heshima kwa hadhi ya binadamu.
“Vile vile Ibara ya 3 ya Mkataba wa Nyongeza wa Maputo inazipa wajibu nchi wanachama kulinda heshima ya utu wa wanawake. Tukio hili pia ni kosa kubwa la jinai la ubakaji wa kundi (gang rape) na kwa mujibu wa sheria yetu ya kanuni za adhabu (Penal Code Cap 16) Kifungu kwa 131A adhabu yake ni kifungo cha maisha,” amesema
Hata hivyo Dk. Henga amesema mbali na ubakaji huo pia kuna makosa mengine ya jinai kama kumwingilia mtu kinyume cha maumbile (unnatural offence) na kusambaza picha chafu mtandaoni ambalo ni kosa la kimtandao.
Henga amewataka watanzania wote kwa umoja kupaze sauti mpaka watu hao wakamate na wachukuliwe hatua kali za kisheria.
“Aidha tunatoa pongezi kwa Boniface Jacob, aliyekuwa Meya wa Ubungo, Dar es Salaam, kwa kutoa taarifa hizi. Tunapongeza Jeshi la Polisi na Waziri Doroth Gwajima kwa hatua za awali walizochukua. Tunakemea vikali wahusika wa kitendo hiki na tunawaasa wananchi kuacha kusambaza video hizo kwenye mitandao ya kijamii ili kumlinda msichana huyo,” amesema Henga
Amesisitiza kuwa jamii ishirikiane na vyombo vya dola na wapenda haki wote katika kuhakikisha haki inapatikana na hatua kali zinachukuliwa dhidi ya waliohusika.