NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WAKALAa ya Barabara Tanzania (TANROADS), imetoa msaada wa vifaa tiba katika kituo cha afya Segerea vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili.
Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na magodoro 10 yenye hadhi ya hospitali na mashuka 74 kwa ajili ya wodi ya wazazi wanaojifungua hospitalini hapo.
Akizungumza leo Julai 2, 2024 kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, Ofisa Rasilimali watu Mkuu Bi. Scolastica Mgaya amesema mbali na ujenzi wa barabara pia wana jukumu la kuisaidia jamii.
“Sisi ni sehemu ya jamii na hizi huduma hazibagui leo tupo makazini ila tukiumwa au wengine pia wakipata na matatizo tutakuja hapa kupata huduma, na leo tumekuja hapa ikiwa tunahitimisha wiki ya utumishi wa umma” amesema Mgaya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kituo hiko, D. Peter Kavishe, amewashukuru Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kwa msaada waliotoa katika kituo hiko kwani vifaa hivyo vitasaidia upande wa wodi ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Pia amesema, suala hilo liwe endelevu na kwenye vituo vya afya vingine ambavyo vinahitaji msaada katika wodi ya mama na mtoto ili kuweza kuisaidia serikali katika sekta ya afya.
Naye, Ofisa Muuguzi wa kituo hiko, Bi. Flora Amos, ameishukuru TANROADS kwa kuwaletea vifaa tiba na kusema kuwa ubora wa vifaa hivi utaongeza ufanisi wa kazi na itasaidia kutoa huduma iliyo bora zaidi.
Wakala ya Barabara Nchini (TANRAODS), imekabidhi vifaa hivyo ikiwa ni kuhitimisha Wiki ya Utumishi wa Umma, ambayo ilifanyika ndani ya wiki mbili.