Lengo ni kujilinda na athari za umeme
*Kapinga ataja juhudi zinazofanywa na Serikali kuimarisha hali ya umeme
Jimbo la Segerea
*Asema usambazaji umeme vijijini unaendelea, vitongoji 4000 kupatiwa
umeme 2024/2025
NA MWANDISHI WETU, DODOMA
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka wananchi
kuchukua hatua za kufunga vifaa vya kuzuia athari za umeme kwenye
nyumba (circuit breaker) ili kujilinda na majanga yanayoweza kutokea
pale umeme unapokuwa mwingi au kupungua.
Kapinga amesema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Segerea,Bonnah Kamoli
aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kwa wananchi wanaopata hasara
kutokana na kukatika kwa umeme au nyumba kuungua.
Kapinga amesema uchunguzi unapothibitisha kuwa tatizo la kuungua kwa
nyumba limesababishwa na TANESCO, Serikali inachukua hatua kupitia
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Akizungumzia hali ya umeme katika Jimbo la Segerea, Kapinga ameeleza
kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme katika jimbo hilo ilitokana na
kuzidiwa kwa kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Gongo la Mboto
ambacho kinapeleka umeme Segerea.
Ametanabaisha kuwa, hali ya umeme Segerea sasa imeimarika kutokana na
Serikali kuchukua hatua ambapo wananchi wengine kutoka Jimbo la
Segerea wanapata umeme kutoka kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha
Kipawa.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia TANESCO pia inatekeleza miradi ya
upanuzi wa kituo cha Gongo la Mboto na ujenzi wa njia ya kusafirisha
umeme kutoka Ubungo hadi Tabata ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa
umeme.
Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini,
Selemani Kakoso aliyetaka kujua mpango wa Serikali kupeleka umeme
kwenye maeneo muhimu katika eneo la Mishamo hasa kwenye Soko na Kituo
cha Afya, Kapinga amesema ni mkakati wa Serikali kuhakikisha umeme
unakwenda kila kijiji na miradi ya usambazaji umeme inaendelea ambapo
kwa mwaka wa fedha 2024/25 vitongoji 4,000 vitapata umeme.
Akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa aliyetaka
kufahamu mkakati wa Serikali kuimarisha umeme kwenye vijiji vya
Namtumbo vinavyopata umeme mdogo, Kapinga amesema Serikali tayari inao
mpango wa kuongeza nguvu umeme kwenye maeneo ya vijijini.