NA MWANDISHI WETU, BARCELONA,HISPANIA
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeshiriki ufunguzi wa Mkutano wa 121 wa Baraza Tendaji la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani ( UN Tourism) unaofanyika leo Juni 11,2024 jijini Barcelona, Hispania huku ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki
Akifungua mkutano huo, Waziri wa Utalii na Viwanda wa Hispania, Jordi Hereu amesema kuwa Shirika la Utalii Duniani linaongeza kasi ili kukamilisha utekelezaji wa Mkakati Endelevu wa Utalii wa mwaka 2030 ambao unalenga kuweka mfumo wa kimataifa wa kutokomeza umasikini uliokithiri, kupambana na ukosefu wa usawa na haki, na kurekebisha mabadiliko ya tabianchi hadi mwaka 2030.
Aidha, amesisitiza kuwa kufuatia utekelezaji huo kumekuwa na mabadiliko ya muundo wa utalii nchini Hispania ili kuthamini utalii endelevu zaidi, unaowajibika na wenye ustahimilivu.
Tanzania ni mwanachama kamili wa Shirika la Utalii Duniani na Mjumbe wa Baraza Tendaji ya Shirika hilo kwa kipindi cha miaka minne (2023 – 2027).
Mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili masuala mbalimbali ikiwemo mwenendo wa sekta ya utalii kimataifa, utekelezaji wa mpango kazi wa shirika hilo, hali ya kifedha pamoja na rasilimali watu.
Aidha, mkutano huo pia utapokea taarifa kuhusu kuanzishwa kwa ofisi za kikanda pamoja na taarifa ya kikosi kazi cha Redesigning Tourism for the Future.