NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TUME ya Nguvu za Atomu (TAEC) imeeleza mafanikio 18 waliyoyapata kwa kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Mafanikio hayo 18 yamebainishwa na Mkurugenzi wa TAEC Profesa Lazaro Busagala leo Aprili 29,2024 wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo Vya Habari jijini Dar es Salaam.
Mafanikio hayo ni kusogeza huduma kwa kujenga Ofisi na miundo mbinu katika kanda ambayo inaipa TAEC uwezo wa kutoa huduma kwa tija na ufanisi.
“Serikali imejenga majengo sita ya Maabara na ofisi katika kanda tano yenye thamani ya takribani Bilion 28.11 ambapo majengo manne kati ya hayo yamekamilika.
“Miradi hiyo ipo Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar.” amefafanua Prof .Busagala
Mafanikio mengine ni makusanyo ya Maduhuli kuongezela kutoka Sh. Bilioni 8.7 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Sh.Bilioni 10.9 mwaka wa fedha 2022/2023.
Mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali ya awamu ya Sita kufungua ofisi za kanda, mipakani na kutumia mifumo ya TEHAMA kama vile TANCIS, TeSWS na EDMS katika kutoa huduma
Kwa upande wa Mazingira ya ufanyaji biashara,Prof.Busagala amesema,TAEC imefanikiwa kupunguza siku za utoaji wa cheti cha uchunguzi wa mionzi (RAC) kutoka zaidi ya siku saba hadi kufikia kwa wastani wa saa tatu hadi siku moja kwa asilimia 98.
Aidha Prof Busagala ameeleza namna TAEC ilivyofanikiwa kuondoa na kupunguza tozo kwa asilimia hadi 100 kwa kuamua kubeba gharama za upimaji (subsidy).
“Hiii ni hasa kwa wale wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kwa kupunguza kutoka asilimia 0.2 ya malipwani kuwa asilimia 0.1 ya malipwani, sawa na punguzo la asilimia 50.” amebainisha Prof. Busagala.
Aidha ameongeza kuwa kwa wafanyabiashara wadogo hupatiwa huduma ya upimaji wa sampuli bure sawa na punguzo la asilimia 100.
Kadhalika Prof Busagala amesema TAEC imefanikiwa kuongeza na kuboresha matumizi ya Tehama ambayo imesaidia katika kufanikisha mambo mengi ikiwemo,Kuunganisha mifumo ya TAEC (EDMS), ifanye kazi kwa pamoja na ile mingine ya serikali mfano GePG, TANCIS, TeSWS yamekuza mawasiliano ndani na nje ya TAEC na kuleta matokeo chanya katika maeneo mbalimbali.
Mbali ya hayo Prof .Busagala amesema Mafanikio mengine ni uboreshwaji wa rasilimali watu ambapo ,Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza idadi ya watumishi wa kudumu kutoka 89 hadi kufikia 142. Kwa kufanya hivyo, TAEC imetekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwahudumia wananchi kwa uharaka zaidi.
“Pia Serikali imetatua tatizo la watumishi wa TAEC kupandishwa vyeo baadhi ya watumishi lililodumu kwa muda mrefu. Watumishi 57 wa TAEC walikuwa na matatizo yaliyodumu kwa muda mrefu lakini Serikali ya awamu ya sita imeyatatua” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo.
Akizungumzia ufadhili wa masomo ya nyuklia,Nje ya nchi Prof.Busagala amesema Serikali ya Awamu Sita kupitia TAEC ipo katika hatua za mwisho kukamalisha mpango wa ufadhili kwa vijana wa kitanzania kusoma vyuo vya nje ya nchi masomo ya teknolojia na sayansi ya nyuklia katika ngazi ya shahada za uzamili.
“Kila mwaka vijana watanzania watano watapata ufadhili huu.Lengo la ufadhili huu ni kuongeza idadi ya wataalam nchini katika nyanja ya teknolojia na sayansi ya nyuklia ili kuhakikisha kwamba nchi inanufaika ipasavyo na fursa za sayansi ya nyuklia” ameeleza
Wakati huo huo Prof.Busagala amesema ,Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TAEC imewajengea uwezo wa kitaalamu watumishi ili kujenga taifa lenye uwezo katika teknolojia ya nyuklia.
Kwa kufuata mpango wa mafunzo uliowekwa na kuanza kutekelezwa, TAEC imeshasomesha 29 na na inaendelea kusomesha wengine 32 ndani ya miaka mitatu. Jumla itakuwa watumishi 61.
Hili ni muhimu sana kwa ustawi wa taifa letu katika sekta ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.
Sambamba na mafanikio yote,ameeleza mafanikio ya trela la kubebea vyanzo vya mionzi ambapo Serikali kupitia TAEC, imebuni na kutengeneza trela maalumu la kubebea vyanzo vya mionzi.
“Awali, watumishi na vyanzo vya mionzi walikuwa wanakaa kwenye gari moja linalotenganishwa na vifaa ambavyo havizuii sawasawa mionzi.
“Jambo hili lilikuwa linahatarisha usalama wa watumishi wanao safirisha vyanzo vya mionzi, wananchi pamoja na mazingira kwa ujumla.
“Trela hili limesheheni vizuizi vya mionzi ili wanasafirishaji na wananchi wasiathirike na mionzi” amefafanua Prof.Busagala
Prof.Busagala amesema ,Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TAEC imeendelea na juhudi za kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyukilia nchini.
“TAEC imefanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanaelewa fursa zilizopo katika matumizi salama ya sayansi ya nyuklia kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
“Ambapo TAEC imeongeza programu za kujitangaza kutoka 12 hadi 60 kwenye Televisheni, Redio, magazeti, mitandao ya kijamii na kushiriki katika maonesho mbalimbali” ametanabaisha Prof Busagala
Prof Busagala ameeleza,Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuongeza tengeo la bajeti ya utafiti kwa TAEC hadi kufikia Sh.Milioni 450 katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema kuwa juhudi hizo zimefanyika ili kupata fursa zaidi za sayansi na teknolojia ya nyukilia na pia kuwalinda wananchi na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi.Katika miaka mitatu machapisho 25 yakitafiti yamepatikana katika juhudi hizi.
Pia ameeleza mafanikio mengine ni ununuzi wa vifaa vya Sayansi na Teknolojia ya nyuklia ambapo,Vifaa vya kisayansi ni nguzo muhimu katika kudhibiti athari za mionzi, tafiti, usimamizi na uendelezaji wa Teknolojia ya Nyuklia.
Amesema ,Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kuweka bajeti na kununua vifaa. Vifaa vya jumla ya Sh.Bilioni . 2.9 B vinaendelea kununuliwa.
Amesema,Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na juhudi za kusimamia udhibiti wa matumizi salama ya mionzi ili kuepuka madhara yake.
“Hadi mwaka 2022/2023 jumla kaguzi 971 kwa mwaka zilifanyika ukilinganisha na kaguzi 244 kwa mwaka 2016/2017. Hili ni ongezeko la asilimia 298.Kaguzi hizi ni nyingi kuliko viwango vya kimataifa vinavyotakiwa”
Pamoja na mafanikio yote Prof Busagala amesema,Katika kudhibiti matumizi salama ya mionzi, Serikali ilifanikiwa kuongeza idadi ya wale wanaopewa leseni kwa asilimia 102 yaani kutoka leseni 297 kwa 2016/2017 hadi wastani wa 767 kwa mwaka.
“Sababu kubwa ya matokeo haya ni ongezeko la juhudi za udhibiti ikiwemo kufanya kaguzi za mara kwa mara, kufungua ofisi mbalimbali na kutumia mifumo ya TEHAMA.”
Prof Busagala amejinasibu kuwa mafaniko mengine ni ongezeko la usimamizi wa matumizi ya mionzi na teknolojia ya nyuklia na Utekelezaji wa nguvu za Atomu namba 7 ya 2003, Serikali imefanikiwa kusajili wataalamu wa mionzi 788 wenye sifa za kutoa huduma ya mionzi kwa watu.
“Ndani ya miaka mitatu, Serikali imesajili wataalamu 1,289 wa kutoa huduma ya mionzi kwa wagonjwa, kutengeneza, kukarabati na kuendesha vifaa vya nyuklia. Jambo hili lilikuwa halifanyiki kwa kipindi cha nyuma.”ameeleza.
Kuhusu mipango ya TAEC,Prof Busagala amesema wataendekea kuwasogezea Wananchi Huduma kwa Kuimarisha Maabara za Kanda na maeneo mengine.
” Serikali itaendelea na juhudi za kujenga uwezo wa watumishi na kusimika vifaa na mitambo husika. Hii ni pamoja na kuendelea kumalizia ujenzi wa maabara na ofisi za kanda zilizo kwenye hatua mbalimbali.
“Ujenzi wa miundombinu unaiwezesha Serikali kusogeza huduma kwa wananchi hivyo kuwa kichocheo kwenye biashara, uchumi, shughuli za wananchi pamoja afya za wananchi na mazingira” amehitimisha Prof.Busagala