- WANAWAKE siku yenu, tambua tunawapenda,
Twatoka matumbo yenu, jueni tunawapenda,
Twanyonya matiti yenu, elewa tunawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Twajengwa malezi yenu, msihofu twawapenda,
Na hata chakula chenu, twakipenda twawapenda,
Sasa leo siku yenu, endeleeni kupanda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Mpate elimu yenu, mbele zidisheni kwenda,
Kulea watoto wenu, jua wote wawapenda,
Kuendesha mambo yenu, mjue tunawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Hebu jifanyie yenu, yale moyo unapenda,
Kama ni miradi yenu, maisha yazidi panda,
Pateni mikopo yenu, twajua mnakokwenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Yafanyeni mambo yenu, familia zitapanda,
Bila ubunifu wenu, jua kwamba tutapinda,
Huo ni wajibu wenu, hata bila ya kupenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Kupitia kazi zenu, na taifa litapanda,
Uchakarichaji wenu, mjue tunaupenda,
Furahieni kivyenu, jua sote twawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Mwapendeza sare zenu, mwapendeza twawapenda,
Ishike nafasi yenu, nasi mzidi tupenda,
Vile ni watoto wenu, kwa malezi mwatulinda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Wengine waume zenu, kutuombea mwapenda,
Hata marafiki zenu, uwepo wetu mwapenda,
Nanyi kwa imani zenu, Mungu zidi kumpenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Kuwapa nafasi yenu, na vile anawapenda,
Maisha ni chanzo chenu, vinginevyo tungepinda,
Twatamba uzazi wenu, dunia mnaipenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda. - Sasa hii siku yenu, tambua tunawapenda,
Ni yetu sherehe yenu, siku hii twaipenda,
Na hamko peke yenu, elewa tunawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
WANAWAKE SIKU YENU, TAMBUA TUNAWAPENDA
Leave a comment