- DUNIA si yako peke, unao pia wenzako,
Ukiyarusha mateke, utaumiza wenzako,
Uwaache wasikike, kulaani mwendo wako,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Waishi nyumba ya pango, na wapangaji wenzako,
Muziki wako ni kigongo, kuzidi hao wenzako,
Sauti yatoa nyongo, hujali hata wenzako,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Huoni hizo kelele, ni karaha kwa wenzako?
Vipi wende wakalale, na hizo kelele zako,
Mbona maisha ya kale, si ujidunge kivyako ?
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Dunia ya kuchangia, wewe na hao wenzako,
Usijekufikiria, kwamba yote hiyo yako,
Wengine nao achia, huo uungwana wako,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Hebu iga kwa wenzako, hawafanyi kama yako,
Wanatambua waliko, hakutaki chokochoko,
Haki za wengine huko, si za kutumbua huko,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Kitimoto wala huko, ni haramu kwingineko,
Kwa hiyo busara iko, inajulikana huko,
Nenda ukale kiliko, usilete kwingineko,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Una nguo nyingi zako, katika kabati lako,
Ruksa vaa kivyako, huo ni uhuru wako,
Lakini wenzako wako, za chumbani si za huko,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Nguo kuvaa chumbani, wawavalia wenzako,
Hujui huo uhuni, wawachefua waliko?
Au hiyo yako dini, yakwambia maandiko?
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Dunia hii ni moja, ya kwetu pia ya kwako,
Ili tuishi pamoja, usitake mambo yako,
Yabakie namba moja, nyuma waweko wenzako,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
- Mambo yetu jumuiya, si ya kwako peke yako,
Sawa na kuimba kwaya, huiwezi peke yako,
Sauti ni nyingi kwaya, wawepo pia wenzako,
Usidhani uko peke, waridhishe na wenzako.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602