NA MAGENDELA HAMISI,DAR ES SALAAM
TAASISI ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU)Mkoa wa Kinondoni imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni watendaji wa Kampuni ya Prezzidar kwa tuhuma za uhujumu uchumi baada ya kupewa jukumu la ukusanyaji ushuru katika masoko ya manispaa hiyo.
Mkuu wa Takukuru Manispaa ya Kinondoni, Ismail Selemani amezungumza hayo leo Februari 6, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 2023 hadi Desemba 2023.
Amebainisha kuwa watendaji hao wamepata tuhuma hizo baada ya kufanyika kwa uchunguzi kwa siku sita na kubainika kampuni yao kudaiwa kufanya udanganyifu wa ukusanyaji na uwasilishaji wa mapato kwenda benki.
“Kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Kinondoni na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hii, tumefanya ufuatiliaji na kubaini kampuni hii ambayo imepewa jukumu la ukusanyaji ushuru wa masoko imethibitika kukusanya na kuwasilisha benki mapato kidogo kuliko uhalisia wake.
“Pia wamekuwa wakikusanya mapato pasipo kutumia POS mashine ipasavyo jambo ambalo ni uhujumu wa uchumi na kuongoza genge la uhalifu na uchepushaji wa mapato ya ushuru, hivyo Januari 10 mwaka huu tukawafikisha mahakamani watendaji wa kampuni hiyo na kufunguliwa kesi Na 1638/2024,” amesema
Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kuzingatia miongozo inayotolewa na Halmashauri na Serikali na kulipa ushuru na kuhakikisha wanapatiwa stakabadhi sawa na kiasi wanacholipa.
Pia ameongeza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni hususan katika Idara ya husika inasimamia kwa karibu wazabuni wote waliopewa dhamana ya ukusanyaji ushuru kwa niaba ya halmashauri.
Aidha ameongeza kuwa katika uzuiaji wa rushwa wamefuatilia utekelezaji wa miradi minne yenye thamani ya Sh.Bil. 7.2 inayoendelea katika hatua ya utekelezaji na kubaini kasoro ndogo ambazo wahusika wameshauriwa kuzirekebisha na kufuatiliwa kwa karibu hadi itakapokamilika ubora kwa thamani ya fedha.
Pia amesema katika kipindi hicho tangu Oktoba hadi Desema 2023 katika programu ya Takukuru rafiki, wamefanikiwa kuzifikia kata nne kupitia vikao vya wadau na kero 10 ziliibuliwa na saba zimepatiwa ufumbuzi.