NA MWANDISHI WETU, DODOMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki kuhusu miradi mbalimbali ya
umeme inayofadhiliwa na benki hiyo pamoja na miradi mingine ya nishati
iliyo katika mpango wa kufadhiliwa.
Mazungumzo hayo ambayo yamefanyika leo Februari 5, 2024 Jijini
Dodoma pia yamehudhuriwa na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na
Taasisi zake wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi
Felchesmi Mramba.
“Benki ya Maendeleo Afrika imeonesha nia ya kuendelea kuiunga mkono
Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo ya
usafirishaji na usambazaji umeme na kubwa zaidi katika hili, wameamua
kuweka kipengele cha nishati safi ya kupikia kwenye mipango yao, na
hii ni katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha asilimia 85 ya
Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.”
amesema Dk. Biteko
Amesema AfDB imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo
mradi wa umeme wa Kakono wa megawati 87.8 kwa kuchangia kiasi cha
Dola za Marekani milioni 161 na mradi wa Malagarasi wa megawati 49.5
kwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 120.
Amefafanua kuwa, Benki hiyo pia imetoa sehemu ya fedha za utekelezaji
wa miradi ya usafirishaji umeme ukiwemo mradi wa
Singida-Arusha-Namanga (kV 400) ambao sasa umefikia asilimia 99, mradi
wa Rusumo-Nyakanazi (94 km) ambao umekamilika kwa asilimia 100 na
mradi wa umeme wa Backbone unaojumuisha ujenzi wa vituo vya kupoza
umeme mkoani Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo kituo cha
Dodoma na Singida vimekamilika kwa asilimia 100.
Kufuatia hatua hiyo, Dk.Biteko ameishukuru AfDB kwa kutoa sehemu ya
fedha ambazo zinatekeleza mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 kutoka
Nyakanazi hadi Kigoma ambao sasa umefikia asilimia 92.
AfDB pia imeonesha nia ya kufadhili mradi wa usambazaji wa Gesi
Asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam kwa
kutumia mfumo wa ushirikiano na Sekta Binafsi (PPP).
Pia AfDB imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali katika mradi wa
njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ya kV
220 sambamba na kushirikiana na serikali katika
uendelezaji miradi mbalimbali ya nishati jadidifu.
Dk. Biteko amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni fursa adhimu
itakayowezesha Taifa kuwa na nishati ya kutosha kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), Kevin Kariuki, amesema nia ya Benki hiyo ni kuhakikisha
miradi ya umeme inayofadhiliwa na AfDB inakamilika kwa wakati ili
kuwapa wananchi umeme wa uhakika.
Ameongeza kuwa, Benki hiyo itaendelea kufanya tathmini kuona namna ya
kuendeleza mipango mbalimbali ya Tanzania kwenye gesi asilia ikiwemo
kupitia mpango mkakati wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) ili kuainisha maeneo zaidi ya ushirikiano.