NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba amesema kuwa suala la amani nchini halinufaishi Serikali au Rais pekee, bali mnufaika mkuu ni kila Mtanzania mmoja mmoja.
Akizungumza katika tamasha la Pasaka la “Mtoko na Christina Shusho” lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Dk. Nchemba alisisitiza kuwa uwepo wa amani ndio unaowezesha shughuli zote za kijamii na kiuchumi kufanyika kwa utulivu.
Alieleza kuwa bila amani, hata matukio makubwa kama tamasha hilo yasingeweza kufanyika, akiongeza kuwa amani ni hitaji la msingi kwa kila mtu, bila kujali nafasi yake katika jamii.
“Amani si kwa faida ya Rais wala Serikali, bali ni kwa kila mwananchi. Hata mchoma mahindi, amani ikivurugika hawezi kutoka kwenda kufanya biashara yake,” alisema Dk. Nchemba.
Aliongeza kuwa hata ibada na maombi hayawezi kufanyika pasipo amani, huku akiwapongeza viongozi wa dini waliohudhuria tamasha hilo kwa kuongoza maombi ya kuliombea taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimpongeza mwimbaji wa nyimbo za injili, Christina Shusho kwa kuandaa tamasha hilo lililowakutanisha waumini mbalimbali kwa lengo la kumsifu Mungu kupitia muziki.
Aidha, alitoa pole kwa wafanyabiashara waliokumbwa na ajali ya moto ulioteketeza soko la Mawasiliano (Simu 2000) lililopo Sinza, akibainisha kuwa Serikali inaendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha tukio hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi alisema kuwa jukumu la kulinda amani linaanzia ngazi ya familia, akiwataka wazazi na walezi kusimamia maadili ndani ya familia zao.
Alisisitiza kuwa taasisi zote za kijamii, ikiwemo dini, zina wajibu wa kushiriki katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa taifa, na si jukumu la Serikali pekee.
“Changamoto nyingi za kiusalama zinaanzia kwenye familia. Familia hujenga jamii, na jamii hujenga taifa,” alisema Katambi, akionya kuwa malezi duni yanachangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.
Katambi alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watanzania kumkumbuka Yesu Kristo wakati wa Pasaka, akieleza kuwa kifo na ufufuko wake ni ishara ya matumaini na mwanzo mpya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema kuwa kifo cha Yesu Kristo ni msingi wa ukombozi wa mwanadamu, huku akieleza kuwa simulizi ya Yuda Iskariote inatoa funzo muhimu kwa jamii ya sasa.
Alibainisha kuwa katika mazingira ya sasa, kila familia inaweza kuwa na changamoto zinazofanana na usaliti, hivyo ni muhimu kuwa na maadili imara ili kulinda mshikamano wa kijamii.




