NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa bila jitihada za makusudi za kuchochea uandishi bunifu na kukuza vipaji vya waandishi chipukizi na wabobezi, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inaweza kukumbwa na changamoto ya kupata vitabu bora vinavyoweza kutumika shuleni.
Profesa Mkenda ameyaeleza hayo leo Jumanne Februari 18,2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa usambazaji wa vitabu vilivyoshinda Tuzo ya Taifa ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Nyerere.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Profesa Mkenda amesema kuwa jukumu la TET ni kuandaa na kusambaza vitabu vya shule ikiwemo vitabu vya kiada na ziada kwa kushirikiana na waandishi wa ndani ili kuhakikisha upatikanaji wa machapisho bora kwa wanafunzi nchini.
Amesema pamoja na kwamba TET inajukumu hilo kuna haja kubwa ya kuibua na kulea waandishi bunifu wa kitanzania ili kuweza kuongeza upatikanaji wa vitabu vyenye ubora vitakavyoweza kutumika shuleni wakati huo huo kukuza lugha ya Kiswahili nchini.
“Bila sisi kuchochea kwa makusudi kuhakikisha kwamba uandishi Pamoja na vipaji vinakuwa kuna hatari sana TET kupata shida ya kuibua vitabu vizuri ambavyo vitatumika huko mashuleni,” amesema Profesa Mkenda
Hata hivyo amesisitiza kuwa kuanzishwa kwa Tuzo hiyo ya Taifa ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Nyerere kupitia TET ni mkakati mahsusi wa kupanua hazina ya vitabu vya ubunifu, akisisitiza kuwa kadiri idadi ya vitabu inavyoongezeka ndivyo mamlaka hiyo inavyopata wigo mpana zaidi wa kuchagua vitabu vinavyofaa kutumika kama vitabu vya kiada na ziada kwa wanafunzi.
Alifafanua kuwa tuzo hiyo pia inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliyekuwa mwandishi mahiri wa mashairi, tenzi na kutafsiri kazi maarufu za fasihi duniani akiwa Ikulu.
Aidha, alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia wazo la kuanzishwa kwa tuzo hiyo mara ya kwanza lilipowasilishwa kwake na hata kuagiza itengewe fedha maalum, hatua aliyosema imeipa tuzo uhai na uhakika wa kuendelea kila mwaka.
Pia ameipongeza Mkurugenzi wa TET, Dk. Aneth Komba kwa kusimamia vyema utekelezaji wa tuzo hiyo na kuhakikisha fedha za tuzo zinaingizwa rasmi kwenye bajeti ya taasisi hiyo ili kudumisha endelevu wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TET, Dk. Aneth Komba amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga kiasi cha Sh. Billioni Moja kati ya hizo Sh. Millioni 400 zilitengwa kwa ajili ya kuchapa na kusambaza vitabu vya washindi wa kwanza wa tuzo hiyo katika kila fani.
Amesema fedha hizo zimetumika kuchapa jumla ya nakala 142,000 ambazo zitasambazwa katika shule zote kwa uwiano wa kati ya vitabu 10 na vitabu 8 kwa shule.
“Aidha, vitabu hivi vimeshapatiwa ithibati ya Kamishina awa Elimu inayoruhusu vitabu kutumika katika shule zetu. Kwa nafasi hii tunaendelea kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutenga fedha za kufanikisha uwepo wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwemo vitabu hivi bunifu,” amesema
Hata hivyo amesema vitabu vilivyozinduliwa leo ni vya aina tatu riwaya, ushairi na hadithi za watoto. Kitabu cha Riwaya kinaitwa Garasa, Ushairi kinaitwa Ngoma ya Muwele na Kitabu cha hadithi za watoto kinachoitwa maziwa ya kuku.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo hiyo, Profesa Penina Mlama, amesema shindano la mwaka huu litafanyika Aprili 13, 2026 na linatarajiwa kuwakutanisha waandishi mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu za ubunifu.
Profesa Mlama amesisitiza kuwa tuzo hiyo inalenga kukuza lugha ya Kiswahili, kuibua na kuendeleza vipaji vya uandishi bunifu, kuhamasisha utamaduni wa kusoma na kujisomea pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta ya uchapishaji nchini.
Ameongeza kuwa mafanikio ya tuzo hiyo yanaonesha wazi kuwa uwekezaji katika fasihi na sanaa ya uandishi si anasa bali ni nyenzo muhimu ya kukuza elimu, utamaduni na uchumi wa maarifa.




