NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Vijana, Joel Nanauka, amesema kuwa kampuni 299 zinazomilikiwa na vijana zimefanikiwa kunufaika na tenda za Serikali kutoka taasisi mbalimbali nchini, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera na mifumo ya ununuzi wa umma inayotoa nafasi kwa vijana.
Nanauka ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa katika bajeti ya Serikali, takribani Sh trilioni 30 hutumika kwenye ununuzi wa umma, hali inayotoa fursa kubwa kwa vijana kujihusisha na shughuli za kiuchumi kupitia kampuni zao.
Amesema Serikali imeendelea kuwahimiza vijana kujisitiri na kujisajili katika mifumo ya manunuzi ya umma, ili waweze kushiriki kikamilifu katika tenda zinazotolewa na taasisi za Serikali.
“Hadi sasa, kampuni 299 za vijana zimefanikiwa kupata tenda kutoka taasisi mbalimbali za Serikali nchini, jambo linaloonesha kuwa mfumo huu unaanza kuleta matokeo chanya,” amesema Nanauka.
Ameeleza kuwa katika ziara zake mbalimbali, ameshuhudia mifano mizuri ya utekelezaji wa sheria ya kutenga asilimia 30 ya manunuzi kwa makundi maalumu, ikiwemo vijana.
“Nimepita maeneo mbalimbali na kuona utekelezaji mzuri, ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Ofisi ya Wilaya ya Same, ambako wanahakikisha wanatenga asilimia 30 ya manunuzi kama sheria inavyoelekeza,” amesema.
Kwa mujibu wa Nanauka, kati ya mwaka 2021 hadi 2025, zaidi ya Sh bilioni 10.8 zimeelekezwa kwa kampuni ndogo ndogo zinazomilikiwa na vijana, hatua inayolenga kuzijengea uwezo wa kukua na kuwa kampuni imara.
Amesisitiza kuwa lengo la Wizara si kuwapatia vijana fedha kwa kiwango kidogo kidogo, bali ni kukuza na kuimarisha kampuni zao ili ziweze kushindana na kutoa ajira zaidi.
“Tunashirikiana na taasisi nyingine za Serikali kuongeza uelewa, kwa sababu dhamira yetu ni kuona vijana wanakuwa na kampuni zenye nguvu na endelevu,” amesema.
Nanauka ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alieleza wazi wakati wa kufungua Bunge mwaka huu dhamira ya Serikali ya kuunda kampuni nyingi za vijana zenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, jambo litakalofikiwa kwa kutumia mifumo rasmi inayowezesha vijana kufanya kazi na Serikali.
Aidha, amesema Serikali imejipanga kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, Toleo la 2024, ili kuhakikisha vijana wanaandaliwa vyema, wanapata fursa za kujiajiri na kuajiriwa.
Amefafanua kuwa mikakati ya Wizara imejikita katika maeneo 13 ya kipaumbele, yakiwemo elimu na mafunzo ya ufundi stadi, ubunifu na uvumbuzi, uchumi wa kidijitali, ukuzaji wa ajira, ushiriki wa vijana katika shughuli za kijamii na kiuchumi, uzalendo na maadili, afya na ustawi, malezi na makuzi, uongozi, mazingira pamoja na usawa wa kijinsia.

