NA MWANDISHI WETU, MWAKITOLYO,SHINYANGA
KUFUATIA maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwasimamia wachimbaji wadogo, Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ipo mbioni kuanza ujenzi wa mtambo wa kuchenjua madini ya dhahabu mkoani Shinyanga.
Hayo yameelezwa leo Desemba , 2025 na Waziri wa Madini,Anthony Mavunde alipofanya ziara ya kikazi na kuzungumza na wachimbaji katika eneo la Mwakitolyo lililopo Shinyanga vijijini.
Waziri Mavunde ametangaza habari hizo njema kuwa, tayari Shirika la STAMICO limeanza utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais na kwamba eneo limeshapatikana katika Kijiji cha Mawemelu na ujenzi utaanza hivi karibuni.
“Mhe. Rais aliona shughuli za uzalishaji mnazofanya hapa Mwakitolyo, akatuelekeza sisi Wizara kupitia STAMICO tulete mtambo wa Serikali hapa ili kuwezesha shughuli za uchenjuaji, mtambo ambao utakuwa na uwezo wa kuchenjua tani 100 hadi 120 za mawe kwa siku”
“Sambamba na hilo, tayari Serikali imenunua mitambo ya uchorongaji 15 kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Hii inaonesha nia thabiti ya Rais wetu Dkt
Samia ya kuwezesha shughuli za uchimbaji mdogo kufanyika pasipo kubahatisha” amesisitiza Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde ameielekeza Tume ya Madini kufuta leseni zote zisizoendelezwa kwa mujibu wa Sheria, kwani watu wengi wamekuwa wakihodhi maeneo na kuzuia fursa kwa wengine wenye uwezo na nia ya dhati ya kufanya shughuli za uchimbaji.
Maeneo hayo yatakayofutwa, tutayawekea mpango na kuyagawa kwenye vikundi vya vijana na wanawake ili wafanye uchimbaji ikiwa ni utekelezaji wa programu ya Mining for a Brighter Tommorow (MBT).
Awali, akieleza juu ya mipango ya Serikali kwa wachimbaji wadogo, Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk. Venance Mwasse amesema mitambo 3 ya uchenjuaji ikiwemo miwili ya dhahabu Mwakitolyo na Buhemba, na mmoja wa Chumvi kujengwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kuhudumia wachimbaji wadogo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mboni Mhita amemshukuru Rais kwa kuendelea kuwashika mkono wachimbaji wa Shinyanga na kusisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na wachimbaji wadogo kutatua kero zao mbalimbali ikiwemo suala la tozo za Halmashauri.









