NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dk. Aneth Komba ameeleza kuwa mabadiliko ya Elimu lazima yaendane na mabadiliko ya teknolojia ili kusaidia ujifunzaji na ufundishaji nchini.
Amesema hayo Desemba 2, 2025 mkoani Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha uhawilishaji (Digitalisation) wa maudhui ya masomo ya Sayansi na Hisabati (STEM) kidato cha pili kwenda kwenye mfumo shirikishi wa kielektroniki utakaosaidia kuboresha Elimu kupitia ujifunzaji na ufundishaji kwa njia ya TEHAMA.
Amesema, Elimu ya Tanzania haiwezi kubaki nyuma kwenye mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanayoendelea Duniani, hivyo kutoa wito kwa Wataalamu hao kuweka jitihada za kutosha ili kupata mfumo bora wenye manufaa kwa Elimu nchini.
Wakati akipita na kukagua kazi zinazoendelea kwenye majopo hayo, Dkt. Komba amewapongeza wataalamu kwa namna wanavyojitoa katika utekelezaji wa majukumu hayo, hasa kwa kuunganisha maudhui ya Elimu ya makundi ya watu wenye mahitaji maalum.
Naye, Mkuu wa Idara ya Teknolojia za Elimu Kwangu Masalu ameeleza mfumo huo utaenda kuongeza ubora wa elimu kupitia ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wa makundi yote nchini.



