NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
WANUNUZI wa madini kutoka maeneo mbalimbali nchini wameendelea kujitokeza katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha, wakikagua na kuhakiki ubora wa madini yatakayouzwa katika Mnada wa Tatu wa Madini ya Vito unaofanyika leo Novemba 27,2025.
Ukaguzi huo ni hatua muhimu inayolenga kuhakikisha uwazi, ushindani na ongezeko la thamani ya madini nchini, kwa kuwa madini yote yatakayopatikana kwenye mnada huo wa kidijitali lazima yakidhi viwango na thamani halisi ya soko.
Mnada huo umeendelea kuvutia wanunuzi wengi wa ndani, jambo linalopanua fursa za kibiashara na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Aidha, unafungua milango kwa wachimbaji na wauzaji kuongeza wigo wa soko kupitia mfumo wa kisasa na salama wa uuzaji.
Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), kuhakikisha mifumo ya usimamizi na mauzo ya madini inakuwa ya kisasa na yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.




