NA FLORAH AMON, DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya Mawasiliano YAS kwa kushirikiana na Mixx, leo imezindua rasmi maandalizi ya mbio za Yas Zanzibar International Marathon 2025, tukio kubwa la michezo litakalofanyika Novemba 23,2025 chini ya kaulimbiu “Kila Hatua ni Special.”
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa YAS, Christina Murimi, amesema mbio hizo zinalenga kuhamasisha afya, utalii, na maendeleo ya jamii kupitia matumizi ya teknolojia na ushirikiano endelevu.

“Kaulimbiu yetu inabeba ujumbe kuwa kila hatua tunayopiga iwe ni kwenye mbio, maamuzi ya maisha au juhudi binafsi ina thamani yake. Kila hatua ni fursa ya kujifunza, kukua na kubadilisha maisha,” amesema Murimi.

Mbio za mwaka huu zitakuwa na makundi matatu ambayo ni Kilometa 5, 10, na 21 ambapo washiriki wote watajisajili na kulipia kupitia mfumo wa kidijitali wa Mixx, unaorahisisha usajili na kuhakikisha kila mshiriki anapokea taarifa muhimu ikiwemo namba ya mbio, uthibitisho wa usajili, na ratiba ya tukio.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio hizo, Ali Said, amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kuwaleta watu pamoja bila kujali umri au hali zao za maisha.
“Kila mshiriki anaposhiriki, anakuwa sehemu ya hadithi kubwa ya Zanzibar – ya afya, mshikamano, na maendeleo,” amesisitiza Said.

Ameongeza kuwa mbio hizo si tu tukio la michezo, bali pia zinachangia kukuza utalii wa michezo na kuendeleza utamaduni wa Zanzibar, huku zikihamasisha matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya maendeleo endelevu.
Aidha, amewataka wananchi wote – vijana, wanawake, familia, na wageni kujisajili mapema kupitia tovuti ya Mixx by YAS, ili kuwa miongoni mwa watakaoshiriki katika tukio hilo la kipekee.

Kampuni ya YAS inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidigitali nchini, ikiwemo mtandao wa 4G na 5G unaofika Unguja na Pemba, ili kuhakikisha kila Mzanzibari anapata nafasi sawa ya kufikia huduma za kisasa za kidijitali.
Kupitia mbio hizi, YAS inathibitisha kuwa teknolojia inaweza kuwa nguzo ya afya, utalii, na maendeleo endelevu ya jamii.
Watanzania wote wanahimizwa kujisajili mapema na kushiriki kwa wingi katika Yas Zanzibar International Marathon 2025, tukio ambalo linaunganisha michezo, teknolojia na utalii, likiwa na kaulimbiu yenye msukumo wa “Kila Hatua ni Special.”

