NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Bodi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari ametoa Tuzo kwa Waandishi wa habari takribani wanane ambao wameibuka kidedea katika Tuzo za uandishi wa habari za hali ya hewa kwa mwaka 2025.

Jaji Bakari amesisitiza Waandishi kuwa habari kuendelea kuandika habari sahihi za hali ya hewa kwa maslahi ya kujenga Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Oktoba 16,2025 baada ya kukabidhi tuzo hizo Mwenyekiti wa Bodi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari amesisitiza waandishi hao wa habari kuendelea kuandika habari sahihi kwa maslahi ya kujenga Tanzania.

Amesema tuzo hizo zinakuwa motisha kwa waandishi hao wa habari katika kuandika habari za Mamlaka ya Hali ya hewa.
“Mliopata Tuzo hizi msibweteke,endeleeni kuandika kadri muwezavyo ili kufahamisha umma wa Watanzania juu ya masuala ya hali ya hewa kwani mafuriko yatakapotokea sio TMA pekee ndo itapata athari bali sisi sote.
“Endeleeni kujiamini na kuandika taarifa sahihi kwa maslahi ya kujenga Tanzania hivyo tunzeni Tuzo hizi kwani ni alama kubwa katika kazi zenu,”amesisitiza.
Jaji Bakari amesema tuzo hizo zinazotolewa na TMA ni kutoa morali kwa waandishi wa habari kuandika kwa wingi habari za Mamlaka hiyo.
Amesema lengo kuu la Tuzo hizi ni kuendelea kuleta hamasa na kujenga umahili katika uandaaji na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa jamii, na kuimarisha mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa.
“Naipongeza TMA kwa kuendelea kuwashirikisha na kutoa motisha kwa wanahabari katika utoaji elimu na usambazaji wa huduma za hali ya hewa nchini na kuhakikisha tuzo hizi zinaendelea kuwa bora zaidi, mwaka hadi mwaka,”amesema
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA ) Dkt.Ladislaus Chang’a amesema Mamlaka yao inaendelea kutambua mchango huu mkubwa wa wanahabari na kuimarisha mahusiano haya kwa kuendelea kutoa motisha mbalimbali kwa wanahabari ikiwemo kutoa mafunzo ya mara kwa mara hususani kipindi cha maandalizi ya utabiri wa mvua za misimu.
Hafla hiyo ilifanyika wakati wa warsha ya wanahabari katika kujadili utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka (Novemba 2025 hadi Aprili 2026).
Miongoni mwa waandishi hao waliopata Tuzo ni pamoja na Penina Malundo,Lisungu Kambona ,Jerome Risasi na Mariam Shabani washindi kwa upande wa Televisheni.
Wengine ni pamoja Mwandishi wa habari kutoka upande wa Zanzibar Amour Khamis Ali huku washindi wa online ni pamoja na Juma Issihaka, Zaitun Mkwama na James Salvatory .

