NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
JUMLA ya miradi 201 ya uwekezaji imesajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji, Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 Julai hadi Septemba 2025 ambapo thamani ya miradi hiyo imefikia zaidi ya dola milioni 2,538.56 za Marekani, sawa na Sh. Trilioni 6.18 za Kitanzania.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatatu Oktoba 6, 2025, Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, amesema kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa na ya kihistoria, hasa ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (TIC) ilisajili jumla ya miradi 256 kwa mwaka mzima.
“Matokeo haya yanaonyesha mabadiliko makubwa katika ufanisi wa usajili wa miradi, hasa katika kipindi hiki cha mpito cha kuunganisha taasisi za uwekezaji chini ya mwamvuli mmoja wa TISEZA,” amesema Teri.
Teri amesema kuwa moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hicho ni ongezeko la miradi ya uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya mauzo ya nje (EPZ) ambapo miradi minane 8 yenye thamani ya dola milioni 97.83 imesajiliwa, na inatarajiwa kutoa ajira kwa zaidi ya watu 2,600 pamoja na kuingiza takribani dola milioni 127.53 za kigeni Ikilinganishwa na miradi mitatu tu iliyosajiliwa mwaka uliopita, ongezeko hili linaashiria kuimarika kwa mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika soko la Tanzania.
Teri ameongeza kuwa miradi inayomilikiwa na Watanzania imeongezeka kutoka 70 mwaka 2024/25 hadi 74 katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ongezeko la asilimia 5.7.
“Hii inaonyesha mwamko mpya wa wananchi kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali, ishara ya kuongezeka kwa uelewa na imani kwa sera za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” ameeleza.
Aidha kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na TISEZA, sekta ya viwanda inaendelea kushika nafasi ya kwanza kwa usajili wa miradi mipya, ikiwa na miradi 85, sawa na asilimia 42.29. Inafuatiwa na ujenzi wa majengo ya biashara (miradi 30, 14.93%) na usafirishaji (miradi 29, 14.43%).
Pia ameongeza kuwa Mkoa ea Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na miradi 79 (asilimia 39.3), ikifuatiwa na Pwani (miradi 29) na Arusha (miradi 16).
Teri amebainisha kuwa wawekezaji wakubwa wanaoongoza kwa mitaji wanatoka katika Falme za Kiarabu (UAE), China, na India, wakichangia zaidi ya asilimia 68 ya thamani yote ya uwekezaji mpya uliosajiliwa.
Katika jitihada za kuendelea kuvutia uwekezaji nchini, TISEZA imezindua kampeni maalum ya kuvutia uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs), inayolenga maeneo matano ya kimkakati: Bagamoyo, Kwala, Benjamini Mkapa Mabibo, Nala na Buzwagi.
Kupitia kampeni hiyo, mamlaka inalenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta za uzalishaji, huku Watanzania wakihamasishwa kushiriki kwa umiliki wa asilimia 100 au kupitia ubia wa angalau asilimia 30.
TISEZA imeeleza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya sera thabiti za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya viwanda, ubunifu na teknolojia.
Kwa mujibu wa TISEZA, Tanzania inajitokeza kama kitovu kipya cha uwekezaji Afrika Mashariki, chenye sera rafiki, miundombinu inayoimarika, na nguvu kazi kubwa ya vijana.
Mamlaka hiyo imetoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hizi za uwekezaji, kushiriki katika miradi ya uzalishaji, na kuwa sehemu ya ajenda ya taifa ya uchumi wa viwanda.
Kwa kiwango cha miradi kilichosajiliwa ndani ya miezi mitatu pekee, TISEZA imeonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza mageuzi ya uwekezaji nchini, hatua inayoiweka Tanzania kwenye ramani ya Afrika kama taifa lenye mazingira thabiti, rafiki na endelevu kwa wawekezaji.
“Ni dhahiri, dira ya uwekezaji wa kisasa inayosimamiwa na TISEZA inalenga si tu kuvutia mitaji, bali kujenga Tanzania yenye uchumi imara, shindani na jumuishi,” amesema Teri.