NA MWANDISHI WETU,KWALA,PWANI
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetenga jumla ya ekari 100 katika eneo la Kwala, mkoani Pwani, kwa ajili ya maendeleo ya viwanda, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kukuza uchumi wa viwanda na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea bandari kavu ya Kwala, Kaimu Meneja wa Mawasiliano kwa Umma na Habari wa TISEZA, Adelina Rushikya, amesema eneo hilo limelenga kuendeleza viwanda vya kimkakati, na kwamba wawekezaji wa Kitanzania watakaotimiza vigezo watapewa ardhi bure kama sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wazawa.
“Mtaji wa chini unaohitajika kwa Mtanzania ni Dola milioni 5 Shilingi bilioni 12.5 huku wawekezaji wa kigeni wakihitajika kuwa na mtaji wa Dola milioni 10 Shilingi bilioni 25 unataka miradi yenye tija, endelevu na inayochangia pato la taifa,” amesema Rushikya.
Amefafanua kuwa eneo la Kwala ni moja kati ya maeneo matano yaliyotengwa nchini kwa uwekezaji wa viwanda, likiwa na mazingira wezeshi kijiografia. Maeneo mengine ni Bagamoyo hekari 151 Nala – Dodoma hekari 67, na Buzwagi hekari 1,333 ambalo linapangwa kwa viwanda vya madini.
Rushikya amesema kuwa kila eneo limepangwa kulingana na fursa na miundombinu iliyopo, kwa lengo la kuchochea viwanda vinavyoendana na mazingira ya kibiashara na kijamii yaliyopo kwenye maeneo husika.
Ameitaja sekta zinazopewa kipaumbele Kwala kuwa ni uchakataji wa mazao ya kilimo, uzalishaji wa dawa, bidhaa za nyumbani, nguo, vifaa vya elektroniki na teknolojia kama vifaa vya jua.
“Tumeanzisha kituo cha huduma kwa wawekezaji (One Stop Center) ndani ya eneo hili ambapo watumishi wapo muda wote kusaidia kuharakisha mchakato wa kuanzisha biashara. Hii ni njia ya kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi,” ameongeza.
Amesema hadi sasa, wawekezaji 10 tayari wameonyesha nia ya kuwekeza Kwala, wengi wao wakiwa ni Watanzania na kwa sasa, wazawa wanapewa kipaumbele katika upangaji wa maeneo lengo lao ni kuwawezesha Watanzania kuwa sehemu ya uchumi wa viwanda.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi kutoka kiwanda cha Snowsea, Gelard Thilya, ambao wanajishughulisha na uzalishaji wa majokofu, amesema wao ni miongoni mwa wanufaika wa kupatiwa eneo la uwekezaji na TISEZA ambapo wameweza kutoa ajira kwa vijana wanaozunguka maeneo hayo ambapo pia bidhaa hizo zinazalishwa na vijana wakitanzania.