NA MWANDISHI WETU,MOROGORO
MENEJA wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Kanali David Mziray amewataka watu mbalimbali kujitokeza kwa wingi kujifunza kucheza mchezo wa gofu ili waweze kuwa wachezaji wazuri na tegemeo kwa taifa.
Kanali Mziray ameyasema hayo Septemba 28,2025 wakati wa mashindano ya raundi ya nne ya kumuenzi mchezaji gofu wa timu ya taifa wanawake marehemu Lina Nkya, Lina PG Tour yaliyofanyika katika Viwanja vya Gymkhana mkoani Morogoro
Amesema awali mchezo wa gofu ulionekana ni wa watu fulani lakini baaada ya hamasa na elimu kutolewa idadi ya washiriki katika mchezo huo imeongezeka hivyo amewataka wanaotamani kujifunza kujitokeza kupata mafunzo katika klabu yao ya Lugalo.
“Mchezo huu wa gofu ni wa watu wote na kuthibitisha hilo klabu ya gofu Lugalo tumeonesha mfano wa kufundisha bure na ukiweza kucheza tunakupa uwanachama kwa muda wa miezi mitatu bure pia ucheze kisha unajiunga na klabu yetu,” amesema Kanali Mziray
Amesisitiza kuwa klabu yao ya Lugalo wanafundisha bure mchezo huo wa gofu na kwamba kwa sasa wana kliniki ya watoto wapatao 72 ambao wanafundishwa kucheza gofu kwa gharama za klabu.
“Pamoja na kufundisha watoto, timu yetu ya gofu ya Lugalo ni timu teule na ipo chini ya usimamizi wa Mkuu wa Majeshi, wachezaji wa timu hii wameendelea kushiriki michuano mbalimbali ya gofu na kufanya vizuri,” amesema
Kwa upande wake Caddy Master, Chiku Elias amesema kuwa mashindano ya Lina PG Tour yameleta ushindani mkubwa na kuendelea kukuza mchezo huo hapa nchini.
Amesema michuano hiyo imekuwa ikifanya kila mwaka na kwamba wameanza hivi karibuni karibuni lakini mwitikio wa wachezaji umekuwa mkubwa kwani wamekuwa waishiriki kwa wingi.
“Tuna tambua kuwa hapo baadae Lina PG Tour itashirikisha wachezaji kutoka nje ya nchi ili kuongeza chachu ya ushindani hapa nchini, tuwaombe wadau waendelee kujitokeza kusapoti michuano hii ili iweze kufanyika mara nyingi,” amesema Chiku