NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SERIKALI na wadau mbalimbali wameombwa kuwaunga mkono vijana katika kuwekeza kwenye ubunifu wanaouanzisha vyuoni, ili kuweza kuleta manufaa kwa jamii na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa Septemba 26, 2025, jijini Dar es Salaam na mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Mohamedi Chipokoso, wakati wa maonesho ya 22 ya Waandisi yaliyofanyika katika viwanja vya Mlimani City.
Chipokoso, ambaye anasomea shahada ya Uhandisi wa Umeme, amebuni mfumo maalum wa kiteknolojia unaoweza kudhibiti vifaa vya umeme majumbani kama vile taa na feni, kwa kutumia simu ya mkononi.
Ameeleza kuwa mfumo huo unamwezesha mtumiaji kuzima au kuwasha vifaa vya umeme hata akiwa mbali na nyumbani kwake, jambo litakalosaidia kupunguza upotevu wa nishati pamoja na kuongeza usalama wa nyumba.
“Mfumo huu ni rahisi kutumia kwa kuwa unaweza kufanya kazi kwa kutumia simu yoyote. Mfano, mtu akitoka nyumbani na kusahau kuzima taa au feni, anaweza kutuma ujumbe mfupi na mfumo utaweza kuzima vifaa hivyo mara moja,” amesema Chipokoso.
Amefafanua kuwa teknolojia hiyo inaweza kufanya kazi hata ukiwa mkoa mwingine au nje ya makazi yako, ilimradi tu mfumo uwe umefungwa nyumbani.
Hata hivyo, Chipokoso ameeleza changamoto zinazowakabili wabunifu wengi nchini, akisema wengi wao hukwama kutokana na ukosefu wa mtaji na wadau wa kuwaunga mkono ili kufanikisha mawazo yao ya kibunifu.
“Wapo vijana wanaoibua mawazo makubwa lakini hukosa msaada wa kifedha na kiufundi kuyapeleka sokoni. Hii ndiyo sababu bunifu nyingi hubaki kwenye karatasi au maabara za vyuo,” amesema.
Aidha, amewahimiza vijana wenzake wenye vipaji kuendelea kubuni bila kukata tamaa, akisisitiza kuwa si kila wazo la ubunifu linahitaji gharama kubwa ili kufanikishwa, na kwamba kuendelea kujaribu ni njia ya kufanikisha ndoto.