NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Uwekezaji Pamoja na Maeneo Maalum ya Uwekezaji (TISEZA) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Benki ya Tanzania Commercial Bank (TCB) kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wawekezaji nchini.
Makubaliano hayo yalisainiwa Septemba 18, 2025 katika Makao Makuu ya TISEZA jijini Dar es Salaam, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, alisema hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi na kuimarisha mfumo wa huduma jumuishi kwa wawekezaji.
“Tumeona busara kushirikiana na TCB kwa sababu ni benki yenye mtandao mpana na inayokua kwa kasi tunataka mwekezaji akifika TISEZA aweze kupata kila huduma kuanzia usajili wa biashara hadi huduma za kibenki katika eneo moja,” alisema Teri.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuziunganisha taasisi za serikali ili kuongeza tija na kupanua wigo wa huduma za kifedha ndani na nje ya nchi.
Aidha, Teri alisema TISEZA na TCB zitaendelea kushirikiana kuhamasisha Watanzania, hususan Diaspora, kuwekeza nyumbani kwani wamekuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kuongeza pato la Taifa.
“Huduma tunazozitoa TISEZA kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji zikikamilishwa na huduma za kifedha za TCB zitawawezesha si tu kuleta fedha zao nchini, bali pia kuwekeza na kunufaika na vivutio tunavyovitoa,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo, alisema benki hiyo imedhamiria kusaidia sekta ya uwekezaji sambamba na kuendelea kukuza huduma zake za kidijitali.
“Mmetupa heshima ya kushirikiana. Tuna matawi 82 na zaidi ya Mawakala 7,000, lakini tunaendelea kukua lengo letu ni kuhakikisha mwekezaji akifikiria huduma za kifedha, benki ya kwanza iwe TCB,” alisema Mihayo.
Mihayo aliongeza kuwa benki yake inaendelea kuwekeza katika teknolojia na inalenga kuongeza idadi ya mawakala kufikia 10,000 ili kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma.
Pia aliahidi kuunga mkono jitihada za TISEZA za kuifanya mamlaka hiyo kuwa kituo cha huduma jumuishi (one stop centre) cha uwekezaji nchini.