NA MWANDISHI WETU, DODOMA
UJUMBE maalum kutoka Serikali ya Uingereza, ukiongozwa na Mkurugenzi mpya wa Maendeleo wa katika Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Anna Wilson, umetembelea Wizara ya Madini na kufanya mazungumzo na uongozi wa wizara hiyo ukiongozwa na Kaimu Kamishna wa Madini, Terrence Ngole.
Ziara hiyo imefanyika leo Septemba 03, 2025 jijini Dodoma ambapo imelenga kumtambulisha rasmi Wilson kwa uongozi wa Wizara ya Madini kufuatia kuanza kwake rasmi majukumu ya kuongoza masuala ya maendeleo kutoka Serikali ya Uingereza hapa nchini.
Wakati wa kikao hicho, ujumbe huo ulipatiwa maelezo ya kina kuhusu muundo wa Wizara ya Madini, taasisi zilizo chini yake, pamoja na majukumu ya Idara Kuu ya Madini.
Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, Kamishna Ngole ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuendelea kudumisha uhusiano mzuri na Serikali ya Tanzania, hususan katika kuendeleza Sekta ya Madini.
Aidha, Kamishna Ngole kwa niaba ya Katibu Mkuu Mhandisi Samamba ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Uingereza kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta hiyo, ikiwemo: uongezaji thamani madini nchini, kuimarisha utafiti na tafiti za kijiolojia, kuboresha miundombinu ya maabara za kisasa, kuwezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ndani katika Sekta ya Madini.
“Tunatambua na kuthamini ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Uingereza, na tunatarajia kuendelea kushirikiana katika kukuza sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa letu,” amesema Ngole.
Ngole ameongeza kuwa moja ya mafanikio ya ushirikiano huo ni kutiwa saini kwa hati ya makubaliano (MoU) kati ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Jiolojia ya Uingereza (British Geological Surrey – BGS), inayolenga kuimarisha utafiti wa kisayansi, huduma za maabara, na kujenga uwezo kwa watumishi wa Sekta ya Madini nchini.
Kwa upande wake,Wilson ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuwa na muundo imara wa kiutendaji na kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuendeleza sekta hiyo kwa uwazi na ufanisi ambapo meahidi kuyafanyia kazi maombi yote yaliyowasilishwa na kusisitiza dhamira ya Serikali ya Uingereza kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa Tanzania katika Sekta ya Madini.
“Tunaamini kuwa kwa kushirikiana, tunaweza kufungua fursa zaidi za maendeleo endelevu kupitia Sekta ya Madini, kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili,” amesema Wilson