NA MWANDISHI WETU,ARUSHA
BENKI ya NMB imewahakikishia wafanyabiashara wakubwa mkoani Arusha ushirikiano wa karibu zaidi katika kukuza shughuli zao, hususan sekta ya utalii, ili kuongeza ufanisi wa kibiashara, mapato na mchango wa taifa katika uchumi wa dunia.
Akizungumza kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyowakutanisha zaidi ya wafanyabiashara 100 wakubwa wa mkoa wa Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema benki hiyo inatambua mchango mkubwa wa Arusha katika sekta ya utalii na biashara kwa ujumla, ndiyo maana imeamua kushirikiana nao kuhakikisha ustawi wa sekta hiyo unazidi kupaa.
“Moja ya jukumu letu ni kuhakikisha ustawi na uendelevu wa biashara zenu. NMB imekuwa ikibuni bidhaa na huduma za kifedha zinazolenga kuondoa changamoto mnazokutana nazo, kuanzia mikopo yenye riba nafuu, teknolojia bunifu za kidijitali, hadi mifumo rahisi ya malipo,” alisema Zaipuna.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, sekta ya utalii imeendelea kuwa kinara katika kuingiza fedha za kigeni nchini, ambapo hadi sasa imefanikiwa kutembelewa na watalii milioni 5.3 iliyoingiza mapato ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 4 na kufanya nchi kuwa miongoni mwa vinara wa utalii barani Afrika.
Zaipuna alisisitiza kuwa mchango wa sekta binafsi, hususan wafanyabiashara wa Arusha, ni nyenzo muhimu kufanikisha malengo hayo.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuendelea kutoa mrejesho wa huduma za benki hiyo na mapendekezo ya bidhaa mpya ili NMB ibuni suluhu zinazokidhi mahitaji yao.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema benki hiyo yenye thamani ya hisa zaidi ya Sh.Trilioni 4, ina uwezo wa kumkopesha mteja mmoja hadi Sh.Bilioni 600.
“Hii ni ishara kuwa tumejidhatiti kikamilifu kutoa masuluhisho ya kifedha, kuanzia mikopo ya uwekezaji, malipo ya kidijitali, huduma za bima na ushauri wa kifedha,” alisema.
Aliongeza kuwa uimara huo umeifanya NMB kutambuliwa kama benki salama zaidi nchini kwa miaka mitatu mfululizo na kushinda mara 11 tuzo ya Benki Bora Tanzania kutoka jarida la kifedha la Euromoney katika kipindi cha miaka 13 iliyopita.
Akieleza huduma zinazolenga sekta ya utalii, Mponzi alisema NMB inatoa mikopo ya kuendeleza biashara za malazi ya wageni, ujenzi wa kambi na mahema ya kifahari (luxury tents), ununuzi wa magari ya usafiri wa watalii pamoja na mikopo ya kulipia vifaa kwa awamu kwa riba nafuu.
Mmoja wa wafanyabiashara waliohudhuria, Frank Kileo, aliipongeza NMB kwa ukaribu wake na wadau wa biashara.
“Tunaona benki yenu imeendelea kuwa kinara licha ya ushindani mkubwa sokoni, jambo linalotupa imani kama wateja wenu, na kujiona tuko salama zaidi hivyo endeleeni kujiimarisha kukabiliana na ushindani uliopo” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa NMB, Baraka Ladislaus, alisema lengo la hafla hiyo ni kusikiliza changamoto za wafanyabiashara, kupata mrejesho wa huduma na kutoa elimu juu ya bidhaa mpya, ikiwemo teknolojia za malipo, kadi bunifu, pamoja na bima za usafiri, afya, mizigo na safari.