NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), ambapo ameisisitiza kuhakikisha inakuwa chachu ya kukuza biashara na kuongeza mapato ya taifa.
Akizungumza leo Agosti 22, 2025 wakati wa hafla ya kuzindua bodi hiyo, Waziri Jafo amesema TanTrade imekabidhiwa jukumu kubwa la kuwa kiunganishi kati ya wafanyabiashara wa ndani na masoko ya kikanda na kimataifa, hivyo bodi hiyo lazima isimamie kwa karibu utekelezaji wa majukumu yake.
“TanTrade sio tu kutafuta masoko ya nje, bali kuhakikisha wafanyabiashara wetu wanapata mazingira bora ya kushiriki kwenye biashara, maonesho na mikutano ya kimataifa. Bodi hii lazima isimamie kwa uadilifu na kufanya mamlaka iwe mfano wa taasisi bora nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa bidhaa nyingi za Tanzania zimeanza kupata nafasi katika masoko ya kikanda na kimataifa, ikiwemo mpunga, mahindi na mchele wa Kahama na Mbeya ambao kwa sasa unauzwa kwa wingi katika nchi jirani.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema bodi hiyo itasaidia kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika biashara na kuongeza ushindani wa Tanzania kwenye soko la kikanda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi mpya, Profesa Ulingeta Mbamba, amesema watahakikisha wanasimamia kikamilifu majukumu ya TanTrade ikiwemo kuimarisha mifumo ya taarifa za biashara, kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, na kutangaza bidhaa za Tanzania ndani na nje.
“Tutahakikisha uwajibikaji, ubunifu na uwazi vinakuwa msingi wa kazi zetu. Hii ndiyo njia pekee ya kukuza biashara ya ndani, ya kikanda na kimataifa kwa manufaa ya taifa,” amesema Prof. Mbamba.