📌 Unahusisha kukuza ujuzi kwa vijana, kuboresha upatikanaji wa huduma
za kifedha, na kuondoa vikwazo vya ujasiriamali
📌 Ataka ujuzi unaotolewa kwa vijana uende sambamba na utoaji wa mitaji
📌 Awaasa Vijana kuwa waaminifu wanapopata nafasi
📌 Wanawake 6,130, Wanaume 4,905 na Makundi maalum 1,226 kufikiwa
NA MWANDISHI WETU, BUKOMBE,GEITA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amezindua
Mpango wa Uwezeshaji wa vijana Kiuchumi (YEE) ambao unagusa maeneo
yanayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki
(EACOP) ikiwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha jamii zilizo karibu
na miradi zinanufaika na miradi hiyo.
Akizindua mradi huo katika Kijiji cha Bukombe, wilayani Bukombe, Mkoa
wa Geita tarehe 18 Agosti 2025, Dk.Biteko amesema mradi huo wa
Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ni moja ya miradi iliyopangwa kuwezeshwa na
Kampuni ya EACOP kwa kipindi cha ujenzi na baada ya ujenzi ikiwa ni
sehemu ya Uwajibikaji wa Kampuni hiyo kwa jamii.
Amesema mradi huo umepangwa kuwafikia zaidi ya vijana 12,261 ambapo
miongoni mwao wanawake ni 6,130; wanaume 4,905 na makundi maalumu ni
1,226 katika awamu ya kwanza inayohusisha Mikoa ya Geita, Kagera,
Tabora na Tanga.
” Tunapozindua mradi huu hatuna budi kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.
Viongozi wetu hawa kwa nia yao ya dhati na moyo wa uzalendo
wameuendeleza na kuusimamia kikamilifu mradi huu wa EACOP ambao
umefikia asilimia 65, tumefikia hapa sababu ya msukumo wao wa
kutekeleza mradi huu ” amesema Dk.Biteko
Ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi wa EACOP mwaka 2022 hadi sasa,
jumla ya Watanzania 9,194 wamepata nafasi za kufanya kazi ndani ya
mradi na hivyo kuwa fursa kwao ya kujipatia kipato, mwaka 2024 kampuni
ilitoa mafunzo maalumu kwa Vijana 170 na kuwapatia kazi kwenye mradi,
Vijana wengine 110 wapo katika masomo na wanatarajiwa kujumlishwa pia
katika Mradi huo pamoja na kutoa
ufadhili wa Vijana 238 katika vyuo mbalimbali nchini.
Amesema wananchi wanaopitiwa na miradi wanayo haki ya kunufaika na
miradi lakini wana wajibu wa kulinda miundombinu ya mradi na kuufanya
kuwa ni sehemu yao kwani unachangia pia kubadilisha maisha ya
wananchi.
Pia, Dk. Biteko ameipongeza kampuni ya EACOP na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) kwa kusimamia kwa ufanisi mradi
huo huku akisisitiza kuwa, ili wananchi waone mradi huo ni sehemu yao
lazima waone faida zake hivyo miradi kama ya YEE inawapa chachu
wananchi kulinda miundombinu ya EACOP kwa wivu mkubwa.
Katika hatua nyingine, Dk.Biteko amesisitiza kuwa, kampuni
mbalimbali zinazotekeleza miradi kuhakikisha kuwa hawaweki mkazo
kwenye kuongeza ujuzi tu kwa wananchi bali wanawapatia mitaji ili
waweze kufanya vizuri zaidi.
Aidha, amewaasa vijana kuchangamkia fursa zinazotokea kwenye miradi,
wajitume, wawe waaminifu pale wanapopata fursa na kueleza kuwa
Serikali itaendelea kuwatengenezea fursa ili wajikwamue kiuchumi na
kuleta maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na
Ajira),Patrobas Katambi amesema Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan
ametengeneza mipango mikakati ya kuhakikisha vijana wanapewa fursa za
ajira na mitaji kwenye maeneo mbalimbali ambapo mpango wa YEE ni
kielelezo cha matokeo ya mipango hiyo.
Ameeleza kuwa, kumekuwa na programu mbalimbali ikiwemo ya uwezeshaji
wananchi kiuchumi ambapo kupitia programu hiyo zaidi ya shilingi
trilioni tatu zilitolewa kwa Watanzania takriban milioni 24 ikiwemo
Wanawake, Vijana na Makundi maalum kwa lengo la kuwawezesha
kujikwamua kiuchumi
Mkuu wa Mkoa Geita, Martine Shigella akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa
Mikoa inayopitiwa na mradi wa EACOP amesema kuwa mradi wa EACOP ni
miongoni mwa miradi mikubwa ambayo wananchi wa Geita wamenufaika nayo
kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira za moja kwa moja na muda na mfupi
pamoja na mnyororo wa thamani kupitia biashara ya vyakula,
mbogamboga, matunda n.k
Amesema Mpango wa uwezeshaji wa vijana kiuchumi ni matunda ya Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuhakikisha vijana wanapata
elimu na ujuzi hivyo mpango wa YEE unaongeza chachu hiyo ya utoaji
elimu na ujuzi kwa wananchi wakiwemo vijana.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema
utekelezaji wa mradi wa EACOP wenye urefu wa km 1443 ni moja ya miradi
17 inayotekelezwa na Wizara ya Nishati ikiwemo mradi wa Julius Nyerere
( MW 2,115) ambao umekamilika, miradi ya umeme ya Ruhudji, Rumakali
na Malagarasi pamoja miradi mingine ya utafutaji na uzalishaji wa
mafuta na gesi asilia ukiwemo wa Eyasi Wembere.
Katika mradi wa EACOP amesema Serikali imechangia shilingi trilioni
1.12 ambazo ni hisa za Tanzania na kuna kampuni za kitanzania 200
ambazo zinafanya kazi mbalimbali katika mradi ambazo zitalipwa jumla
ya shilingi trilioni 1.325 ikiwa ni moja ya matunda ya uwepo wa mradi
huo nchini.
Akieleza sababu za kufanyika.kwa uzinduzi wa mradi wa YEE wiiayani
Bukombe amesema kuwa Bukombe kuna kituo kikubwa zaidi cha kusukuma
mafuta yatakayotoka nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga, kuna kambi
kubwa ya mradi wa EACOP na pia kilometa 20 za bomba hilo la mafuta
zinapita katika eneo la Bukombe.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
( TPDC), Mussa Makame ameeleza kuwa, TPDC imeendelea kushirikiana na
kampuni ya EACOP kuhakikisha kuwa mahitaji ya wananchi yanabainishwa
na kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii
(CSR).
Ameeleza kuwa mahitaji yaliyoainishwa katika mradi wa YEE yaliandaliwa
kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa kwa ngazi ya vijiji, Kata na
Halmashauri zilizopo maeneo linapopita bomba la mafuta.
Awali Clare Haule, Meneja wa Uwekezaji na Uwajibikaji kwa Jamii
katika kampuni ya EACOP alisema mradi wa YEE umeanzishwa kwa kutambua
kwamba zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya watu wa Tanzania ni vijana
chini ya umri wa miaka 35. Hata hivyo, vijana wengi hasa katika maeneo
ya vijijini wanakumbana na vikwazo vingi kama vile ukosefu wa ajira,
ukosefu wa mafunzo ya ufundi stadi , na ugumu wa kupata mitaji ya
kuanzisha au kukuza biashara.
Alisema awamu ya kwanza ya Mradi wa YEE utawawezesha kiuchumi vijana
katika mikoa ya Geita, Kgera,Tabora, na Tanga na mikoa inayobaki
itanufaika katika awamu ya pili ambayo ni Singida, Shinyanga, Dodoma
na Manyara ambapo vijana watapewa ujuzi unaolingana na mahitaji ya
soko, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuondoa vikwazo
vya ujasiriamali na ajira binafsi.
Aliongeza kuwa, Mradi wa YEE ni sehemu ya Sera ya Uendelevu ya EACOP,
chini ya nguzo ya Vizazi Vijavyo, inayolenga kujenga uwezo wa vijana
na kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi katika jamii zinazoguswa
na mradi.