NA MWANDISHI WETU, ANTANANARIVO, MADAGASCAR
TANZANIA imepongezwa kwa utendaji mzuri wa kushughulikia changamoto za kiusalama katika kanda ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), baada ya kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 15, 2025, wakati wa Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaofanyika Madagascar chini ya mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi Kombo alisema katika uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Tanzania iliongoza juhudi za pamoja za kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya kikanda, kuimarisha utawala wa kidemokrasia na kuimarisha miongozo ya kulinda amani.
Hayo yalifanyika chini ya uongozi imara wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
Katika kipindi cha mwaka mmoja, Tanzania iliitisha mikutano mitano ya dharura ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kujadili na kushughulikia changamoto za kiusalama zilizokuwa zikiibuka katika kanda.
Kiatika kipindi hicho pia, Tanzania iliongoza timu ya SADC ya waangalizi wa uchaguzi katika nchi za Namibia, Msumbiji, Mauritius na Botswana. Timu hizo ziliongozwa na watu maarufu kama vile Rais Mstaafu wa Zanzibar,Amani Abeid Karume na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Peter Pinda ili kuhakikisha kuwa uchaguzi wa haki, huru na wazi unafanyika katika nchi hizo.
Balozi Kombo alisema juhudi za kutafuta amani zilifanyika za njia tofauti zikiwemo za kidiplomasia au kutuma vikosi vya kulinda amani, hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ((DRC).
Kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa wakuu nchi za EAC na SADC na kutuma vikosi vya kulinda amani mashariki mwa DRC na baadaye kuondolewa ni kudhihirisha namna nchi za SADC zilivyojipanga kutafuta ufumbuzi wa migogoro yake.
Balozi Kombo alimalizia hotuba yake kwa kutahadharisha juu ya matishio mapya yanayoibuka duniani kama vile ugaidi, uhalifu wakimtandao, uhalifu unaovuka mipaka na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema changamoto hizo zinahitaji juhudi za pamoja na mbinu za kisasa kuzikabili, vinginevyo athari zake zitakuwa kubwa katika kanda.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Mulambo Haimbe; Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi na Mwenyekiti ajaye,Nancy Tembo na Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi ambaye atawasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa masuala ya amani, ulinzi na usalama na na wajumbe watapata fursa ya kuijadili.