*AAHIDI MSHIKAMANO KWA MGOMBEA UBUNGE ATAKAYECHAGULIWA
NA MWANDISHI WETU, KYELA,MBEYA
ALIYEKUWA Mtiania,Jimbo la Kyela,mkoani hapa Godlove Mwakibete ‘Chief Godlove’, amerudi kuwashukuru wananchi wa Kyela kwa imani waliomuonesha baada ya jina lake kukatwa na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi kwenye mchakato wa kuwania ubunge.
Mwakibete ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kusaidia Yatima, Wajane na watu wasiojiweza ya ‘Chiefgodlove foundation’,alikutana na wananchi hao katika viwanja vya Kyelucu vilivyopo Ipinda mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kutoa shukrani hizo kwao.
Katika hotuba yake amesema licha ya jina lake kutorudi lakini ndoto zake za kuendelea kuiletea maendeleo Kyela zipo palepale.
“Kukatwa jina langu katu hakuwezi kunirudisha nyuma katika kufikiria maendeleo ya wanaKyela, kupitia marafiki zangu na wadau mbalimbali tutaendelea kutafuta fursa kila zitakapoonekana ili Kyela iweze kusonga mbele na kuwa Jimbo la mfano kuigwa.
“Binafsi naamini katika mchakato huo wa uchaguzi safari hii haikuwa bahati yangu na kama nimekosa leo basi nitapata kesho ,niwashukuru sana kwa imani mlionionesha kwangu na ninaahidi nitaendelea kuwa nanyi bega kwa bega kwa kila jambo,”amesema Mwakibete.
Aidha ameeleza kuwa ndoto zake wakati wa kutaka kiti hicho cha Ubunge ilikiwa ni kuwaletea vijana maendeleo na kubwa suala zima la upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo kuwa na bima ya afya kwa kila mwananchi.
Hata hivyo amesema anaamini ndoto hizo zitawezekana kwa kushirikiana na atakayechaguliwa kwa kuwa anaamini naye malengo yake ni kuibadili Kyela na si vinginevyo.
“Pia nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipokishukuru Chama changu, naahidi kutoa ushirikiano kwa Mgombea wetu wa Urais,Rais Samia Suluhu Hassan na chama kwa ujumla na nina ahidi kuwapa ushirikiano pale itakapohitajika kufanya hivyo.
“Mwisho naomba wanaCCM kuelekea uchaguzi mkuu tushikamane kwa kuondoa tofauti zetu na kuwakubali watakaopitishwa na uongozi wa juu wa chama ndio wamestahili na sisi kazi yetu iwe kuwapigia kampeni ili tupate kura nyingi za ushindi sio zao tu bali na chama kwa ujumla,”amesema Godlove
Kwa upande wao wananchi, akiwemo Atupile Mwakifulefule, amesema Godlove walitegemea angerudishwa kwa kuwa walimuona anastahili kutokana na ndoto alizokuwa nazo kwao vijana lakini ndio hivyo chama kimeamua kumuweka kando kwa taratibu zao na wao hawawezi kuwapinga.
Naye Charles Melkyori, amesema chama kisiache kuwatumia watu kama wakina Godlove kwa kuwa kuisaidia jamii inatoka moyoni mwao na sio kwamba alikuwa anafanya hivyo ili kufukuzia madaraka.
“Huyu kijana tulimpenda kwa kuwa hajaanza kuisaidia jamii jana wala juzi,tunamuona namna anavyoguswa na matatizo ya watu huko uraiani,hiki ndicho wananchi tunachohitaji,”amesema Melkyori.