NA MWANDISHI WETU DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mhandisi Zena Said amewataka viongozi kuwa na malengo ya kuleta mabadiliko chanya katika maeneo wanayoyasimamia pamoja , huku wakifungua uwezo wa timu zao kwa kuwasaidia wengine kufikia malengo yao.
Mhandisi Said aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya kwanza ya jumuiya ya wahitimu wa Taasisi Uongozi (alumni), iliyowajumuisha zaidi ya watu 865.
Alisema ni muhimu viongozi kuhakikisha wanakuwa daraja kwa wengine kwa kuwasaidia wanaowasimamia kufikia malengo yao hasa ya kuboresha kazi zao.
“Kwa kutumia uongozi bora, Afrika inaweza kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zake za maendeleo, lakini pia tukiwa na viongozi wazuri ambao wanawasaidia wengine tunaweza kufikia malengo makubwa ambayo tumejiwekea,” alisema
Hata hivyo alisema kuwa zaidi ya miaka kumi na mitano iliyopita, Serikali ya Tanzania ilitambua umuhimu wa uongozi na maendeleo ya uongozi katika kuleta maendeleo endelevu nchini, na hivyo kuanza kuchukua hatua madhubuti kuanzisha kituo maalum cha kushughulikia masuala hayo.
Alisema kuwa kupitia Mchakato wa Helsinki, ambapo ilipendekezwa kuanzishwa kwa kituo cha kikanda cha kukuza maendeleo ya uongozi barani Afrika, Tanzania iliona fursa hiyo kama ya dhahabu na kuchukua jukumu hilo kwa niaba ya Afrika.
“Tuliona huu kama wakati wa dhahabu wa kusukuma mbele ajenda ya uongozi, na Tanzania ikachukua jukumu hilo kwa ujasiri,” alisema Mhandisi Said
Alieleza kuwa katika safari hiyo, Serikali ya Finland imekuwa mshirika mkuu wa maendeleo, na msaada wake umekuwa wa maana kubwa katika kufanikisha shughuli za Taasisi hiyo kwa kipindi chote cha miaka kumi na mitano.
“Ningependa kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Finland kwa msaada wake wa miaka kumi na mitano. Mchango wao endelevu umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Taasisi,” aliongeza.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuishukuru Umoja wa Ulaya kwa kuwezesha kupanuka kwa Mpango wa Uongozi wa Wanawake ambao umekuwa ukitekelezwa na Taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Mhandisi Said alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Uongozi imejipambanua kuwa kinara wa kukuza uongozi wenye mwelekeo wa maendeleo endelevu barani Afrika.
Alisema taasisi hiyo imekuwa ikilenga kuwawezesha viongozi wa Afrika kuleta mabadiliko chanya, kuchochea ubunifu, na kujenga mazingira ambayo kila mmoja anathaminiwa na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo.
Akizungumzia kuhusu jumuiya hiyo ya wahitimu wa taasisi hiyo (alumni), Said alisema kuwa wahitimu wa Uongozi wanajumuisha zaidi ya watu 865 kutoka sekta mbalimbali za bara la Afrika, jambo ambalo linaakisi nguvu ya utofauti wa kijinsia, sekta, utaifa na tamaduni.
“Kinachonivutia zaidi kuhusu wahitimu wa Uongozi ni utofauti wao. Utofauti huu unaongeza thamani kwa kutoa mitazamo mipya, kuvunja dhana potofu na kuleta fursa mpya za ukuaji na ubunifu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Kiongozi huyo aliwataka wahitimu kuendeleza uhusiano wao na Tassisi ya Uongozi kupitia ushiriki wao katika programu mbalimbali kama vile elimu kwa wakuu wa taasisi, mijadala ya sera, tafiti, na uzalishaji wa maarifa.
“Jitokezeni kutoka katika maeneo yenu ya faraja. Kutana na wahitimu wengine, jengeni mitandao ya kitaaluma. Toeni utaalamu wenu kwa wanafunzi wa sasa, ikiwemo kuwa washauri wao,” alihamasisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Uongozi ,Kadari Singo alisema kuanzisha kwa Jukwaa hilo la wanajumuiya waliohitimu kozi mbalimbali za Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kurudisha kile walichokipata katika taasisi ya Uongozi na kurudisha kwa jamii.
”Kwa jumla waliohudhuria zile programu za muda mrefu hadi sasa ni 860,na leo hapa tumefanikiwa kupata wanajukwaa 400 waliokuja katika uzinduzi huu wa jukwaa.
”Lengo hasa la uwepo wa jukwaa hili ni kuona kwa namna gani wahitimu hao wanaweza kurudisha kile walichokipata kutoka katika Taasisi yetu kwa jamii na kuona wanashirikianaje,”alisema
Aidha Singo alisema Taasisi ya Uongozi inatarajia kuanzisha programu nyingine mpya ya viongozi Chipukizi ambayo itaanza kuwaandaa viongozi mapema hususan wakiwa wachanga ili wanapokuja kushika nafasi waweze kutumikia vema.
”Wakati mwingine viongozi wanalewa madaraka kwa sababu umempa nguvu na sio ujuzi,matokeo yake anatumia nguvu na sio ujuzi alioupata katika mafunzo kama haya.
”Hili Jukwaa la wahitimu waliomaliza mafunzo ya uongozi watakuwa sehemu yakuwajengea uwezo hawa chipukizi,ambapo utakuwa ni mfumo ambao wale waliotangulia wawe wanawaongoza viongozi hao chipukizi,”alisema
Singo alisisitiza kuwa Jukwaa hili sio la taasisi bali ni la wanajumuiya wenyewe ila kwa kuanza litakuwa linawakutanisha wahitimu hao kwa mwaka mara moja kwa lengo la kubadilishana uzoefu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Uongozi,Ombeni Sefue alisema mafanikio hayo yote ya Taasisi ya Uongozi yametokana na msaada wa wazi na endelevu kutoka kwa Serikali ya Tanzania na Finland.
”Niwapongeze wakurugenzi wa Bodi waliopita na waliopo sasa,pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Uongozi,Washauri,Wakufunzi na Wadau wa Maendeleo Umoja wa Ulaya,”alisema.