NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa hadi kufikia Juni, 2025 benki hiyo ilikuwa imenunua jumla ya Tani 6.6 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 707.6 sawa na Sh. Trilioni 1.8 za Kitanzania.
Tutuba ameyasema hayo leo Julai 30,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) uliotengenezwa na wataalamu wa BOT kwa kushirikiana na wataalamu wengine waliopo hapa nchini.
Amesema kwa mwaka 2024/2025 serikali ilifanya marekebisho ya sheria ya madini na kuiwezesha BOT kuanza ununuzi wa dhahabu kwa kutumia fedha za ndani na kwamba kiasi hicho cha dhahabu walichonunua ni sawa na asilimia 110 ya lengo la kununua tani 6 kwa mwaka 2025.
“Hata hivyo Benki Kuu imeendelea kununua dhahabu na hadi Julai 29, mwaka huu kwa maana ya jana tulikuwa tayari tumefikisha jumla ya tani 6.8 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 731,” amesema Tutuba
Aidha amesema kwa upande wa thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika ambapo kwa mwaka ulioishia hadi Julai 29, 2025, shilingi hiyo imeimarika kwa wastani wa asilimia 4.7 na hivyo kufanya kiwango cha kubadirishia Dola moja ya Marekani kufikia Sh. 2550.72 kwenye soko la jumla na Sh.2590.3 kwenye soko la rejareja.
“BOT tunaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuongeza ukwasi na kuboresha usimamizi wa masoko ya fedha ili kuimarisha zaidi thamani ya shilingi yetu kulingana na ukuaji wa uchumi,” amesema
Aidha amesema Benki Kuu imeendelea kusimamia biashara ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni ambapo kwa mwaka 2023 ilifanya marekebisho ya kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara ya kubadilishia fedha za kigeni na kuongeza wingi wa huduma kwa wananchi na wageni wanaokuja hapa nchini.
Tutuba amesema hadi kufikia Juni, 2025 jumla ya maduka yenye leseni ya kuendelea kutoa huduma hiyo ya kubadilisha fedha za kigeni yamefikia 174, huku jumla ya benki za biashara 37 zinaendelea kutoa huduma hiyo ya kubadilisha fedha za kigeni kupitia matawi yao yaliyopo nchi nzima.
Hata hivyo amesema hadi kufikia Juni mwaka huu akiba ya fedha za kigeni imefikia jumla ya Dola za Kimarekani Bilioni 6.1 ikiwa ni kiasi cha juu kuweza kufikiwa kwa nchi.
Kuhusu mfumuko wa bei
Tutuba amesema mfumuko wa bei nchini umeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 4.8 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 3.2 mwaka 2024 na katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025 wameendelea kuwa na mfumuko wa bei wa wastani wa asilimia 3.2.
“Kiwango hiki kinaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache duniani zenye mfumuko wa bei ndogo ikilinganishwa na wastani wa dunia wa asilimia 4.7 kwa mwaka 2024. Aidha maboresho ya sera ya fedha yaliyofanyika Januari 2024 kwa kuacha utaratibu wa ujazi wa fedha na kuanza kutumia riba ya Benki Kuu katika kudhibiti mfumuko wa bei imekuwa miongoni mwa nguzo imara,” amesema