* ATEMBELEA KIWANDA CHA DAWA NA ZANA ZA KILIMO NCHINI BELARUS
*WASHUHUDIA UTIAJI SAINI HATI TATU ZA MAKUBALIANK NA MKATABA MMOJA
NA MWANDISHI WETU, MINSK,BELARUS
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin na kujadiliana naye masuala ya uwekezaji, biashara, nishati, madini, elimu, afya, teknolojia na kilimo kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumanne, Julai 22, 2025) ofisini kwa mwenyeji wake, mtaa wa Sovetskaya, jijini Minsk.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza mwenyeji wake kuwa, mbali na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia anataraji kuwa ziara hiyo itaongeza chachu ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji, elimu, afya na upatikanaji wa zana za kisasa kwenye kilimo kutokana na fursa mbalimbali zilizoko nchini.
Amesema mazungumzo yao yamefungua milango ya kuimarisha uwekezaji, fursa za biashara na masomo katika vyuo vya elimu ya juu, na kwamba wamekubaliana na mwenyeji wake kuwa Mawaziri wake na Naibu Makatibu Wakuu walioko kwenye ziara hiyo wakutane ili kuanza majadiliano rasmi ya kufanikisha nia ya kampuni ya Minsk Tractor Plant OJSC ya kuleta kiwanda kama hicho nchini.
Amewaeleza baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wanaotoka Chama cha Wafanyabiashara cha Belarus kwamba hivi sasa Tanzania imepunguza muda wa kupata leseni, imeongeza maeneo ya uwekezaji (TISEZA) na imeboresha sheria za kikodi ili kuhamasisha uwekezaji nchini.
Amewaeleza fursa nyingine za kuwekeza Tanzania ni uwepo wake kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya kikanda ya SADC na Eneo Huru la Biashara barani Afrika (ACfTA) pamoja na uwepo wa nchi sita zinazoizunguka Tanzania na hazina bandari (land-locked countries) ambazo zina wakazi wengi.
Katika kikao hicho, Mawaziri Wakuu wote wawili walishuhudia utiaji saini wa hati tatu za makubaliano na maktaba mmoja baina ya mawaziri wa nchi hizo mbili. Hati hizo zilizosainiwa leo zinahusu mashauriano ya kisiasa; makubaliano ya kuendeleza sekta ya kilimo na sekta ya elimu.
Aidha, mkataba uliosainiwa leo ni baina ya Chama cha Wafabiashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania (TCCIA) na Chama cha Wafanyabiashara wa Belarus unaolenga kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kufanya ziara ya Kiserikali nchini humo na kuipa heshima nchi hiyo kupokea kiongozi mkuu kutoka Tanzania kwa mara ya kwanza.
Amesema Belarus inaiona Tanzania kuwa mdau muhimu wa ushurikiano katika nyanja mbalimbali na hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo inao utaalamu (expertise) katika nyanja nyingi ambazo zimegusiwa wakati wa majadiliano yao.
“Tuko tayari kutoa ushirikiano kwenye maeneo uliyoyataja na wala sioni haya kusema hivyo kwa sababu nchi yetu inao utaalamu mkubwa kwenye maeneo uliyoyaainisha,” amesema.
Amesema mazungumzo yaliyofanyika leo baina ya viongozi hao wakuu ni mwanzo wa ushirikiano wa kudumu ambao utasaidia kukamilisha masuala yaliyoibuliwa kutokana na ziara hiyo
“Ziara hii ni fupi na hatuwezi kukamilisha kila jambo, lakini maeneo yote ya usalama wa chakula, utoaji wa huduma za tiba, kilimo na elimu yanaweza kukamilishwa na timu zetu,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kumtakia heri Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Mapema asubuhi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea kiwanda cha kutengeneza dawa cha Republican Unitary Production Enterprise “Belmedpreparaty” na kiwanda cha kutengeneza matrekta na zana za kilimo cha Minsk Tractor Plant OJSC.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Shariff Ali Sharriff, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk. Khatibu Kazungu pamoja Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Dk. Stephen Nindi.
Wakati huo huo, Majaliwa, leo Julai 22 J2025, ameendelea na ziara yake rasmi nchini Belarus kwa kutembelea maeneo muhimu ya uzalishaji na ushirikiano wa kimkakati.
Akiwa katika mji wa Minsk,Majaliwa alitembelea kiwanda cha Belmedpreparaty, ambacho ni maarufu kwa utengenezaji wa dawa za binadamu.
Aidha, Waziri Mkuu pia alitembelea kiwanda cha Minsk Tractor Plant, ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa matrekta na mitambo ya kisasa ya zana za kilimo. Ujumbe wa Tanzania ulijionea teknolojia ya hali ya juu inayotumika katika uzalishaji wa vifaa hivyo.
Wakati wa ziara hiyo, pamoja na viongozi wengine, Waziri Mkuu aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Cosato Chumi.
Majaliwa pia aliweka shada la maua katika mnara wa mashujaa wa Jamhuri ya Beralus.
Kwa ujumla, ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania kuimarisha mahusiano ya kimataifa kwa manufaa ya wananchi, hasa katika sekta muhimu za maendeleo kama afya na kilimo.