NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MASHINDANO ya Gofu kwa ajili ya kumuenzi mchezaji wa zamanı wa timu ya taifa ya wanawake ya gofu, marehemu Lina Nkya msimu wa nne yamezidi kuchanja mbuga huku mchezaji wa wakulipwa kutoka klabu ya gofu Gymkhana Dar es Salaam, Fadhil Nkya akiibuka tena mshindi wa kwanza na kujipatia kitita cha Sh. Milioni 6.8.
Michuano hiyo ambayo ilifanyika katika katika Viwanja vya Lugalo Gofu jijini Dar es Saaalm kuanzia Julai 17 hadi 20, 2025 iliwakutanisha wachezaji zaidi ya 150 na Nkya amezidi kuonesha umwamba wake kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa na kufanya kushika nafasi hiyo kwa mara ya sita mfululizo.
Akizungumza mara baada ya kuibuka mshindi wa mashindano hayo kwa upande wa wachezaji wa kulipwa, Nkya amesema amekuwa mshindi wa mashindano hayo mara ya sita mfululizo na kwamba siri kubwa ya mafanikio yake ni mazoezi bila kuchoka wala kukata tamaa.
Alisema Lina PG Tour imekuwa ni moja ya mashindano muhimu yanayowaleta wachezaji pamoja na kuwafanya wafanye mazoezi kwa bidii ili kujiweka katika viwango bora vya kwenda kushindana na mataifa mengine.
“Lina PG Tour kila mwaka inakua na kuleta mabadiliko katika mchezo huu wa gofu nchini, namshukuru Mungu kwa kuendelea kufanya vizuri katika michuano hii, binafsi mimi ni mwalimu nimekuwa nikiwafundisha wachezaji chipukizi namna ya kucheza mchezo huu ili na wao hapo baadae waje kuchukua nafasi zetu na kupeperusha vema bendera ya nchi,” amesema Nkya
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mshindano hayo na Mkuu wa familia ya Nkya, Said Nkya amesema kuwa mashindano hayo yalikuwa ni kwaajili ya wachezaji wa gofu wa kulipwa na ridhaa lakini wamewaingiza wachezaji wasindikizaji ili kukuza pia vipaji vyao.
Aidha amesema kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitatu ya michuano hiyo wameamua kuanzisha mashindano mengine ya gofu kwa ajili ya watoto wadogo yatakayoitwa ‘Lina Junior Tour’ lengo ni kuwafundisha watoto hao ili waje kuwa wachezaji wazuri.
“Katika Lina Junior Tour tutakuwa na mashindano matatu kwa mwaka lengo tunataka kuwakuza hawa watoto ili wapate uzoefu wa kutosha, washindi wa kwanza hadi tano tutawachukua na kuwaleta katika shindano hili kubwa, tunafanya hivyo kwa sababu tunajua hawa waliopo wanazidi kukua na kuzeeka hivyo ni lazima kuwaanda watoto watakaokuja kuwarithi,” amesema
Naye kapteni wa klabu ya gofu ya TPDF Lugalo, Meja Japhet Masai amewapongeza waandaaji wa mashindano hayo ambayo amesema kwa mara ya kwanza yamefanyika katika klabu hiyo ya Lugalo kwa weledi mkubwa.
“Watu wamejitokeza kwa wingi na tumejifunza mambo mengi hasa ushirikiano ulioneshwa, tumeshuhudia uimara wa uwanja wa Lugalo hivyo tunawapongeza wale wote walioshinda na kuwataka ambao hawakushinda kujipanga upya na mashindano yajayo,” amesema Meja Masai
Mbali na Nkya kushika nafasi ya kwanza, mshindi wa nafasi ya pili ni Abdallah Yusuph aliyepata Milioni 4.3 na mshindi wa tatu Nuru Mollel aliyepata Milioni 3.4.
Kwa upande wa wachezaji wa ridhaa (Elites), mshindi wa kwanza ni Prosper Emmanuel aliyepata kiasi cha Sh. Milioni 2.2, nafasi ya pili ikichukuliwa na wachezaji wawili waofungana pointi ambao ni Julius Mwinzani na Gabriel Abel ambapo kila mmoja amepata Milioni 1.1.
aliyepata Milioni 1.3, namba tatu ni Gabriel Abel aliyepata 900,000.
Kwa upande wa wachezaji wasindikizaji mshindi wa jumla ni Ally Mwinyi, mshindi wa pili katika kundi hilo ni Maryanne Mugo, huku makundi maalum, mchezaji bora wa jumla kwa wanaume ni Abid Omari na kundi la wanawake ni Amina Nkungu.
Mshindi katika kundi la wanaume daraja A wa kwanza ni Nicholous Chitanda huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Sigfrid Urassa, katika kundi la wanaume daraja B nafasi ya kwanza ni Shukuru Sanga huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Kennedy Kajuna