NA MWANDISHI WETU,KAKONKO,KIGOMA
MENEJA wa Mamlaka ya Maji (RUWASA) wilayani Kakonko mkoani hapa Benjamin Mujuni(48) na fundi sanifu wa maji Denis Manji (36)wamefikishwa Mahakama ya wilaya kwa kosa la uhujumu uchumi.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani Julai 15 mwaka huu kwa shauri hilo la uhujumu uchumi lililosajiliwa kwa namba 17155/2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Maila Makonya
Kwa upande wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( TAKUKURU)shauri hili linaendeshwa na Wakili wa Serikali Augustino Lohay
Mujuni na Manji wanashtakiwa kwa Matumizi mabaya ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22, Ubadhirifu na ufujaji kinyume na kifungu cha 28 (1), vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, vikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga Sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022 na kosa la kughushi kinyume na kifungu cha 333, 335(a) (d )(i)(ii) na 337 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 kama ilivyorejewa 2022.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba washtakiwa hao wamefanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha Sh. 9,970,000 zilizotolewa kwa ajili ya kuwezesha shughuli za maadhimisho ya wiki ya Maji wilaya ya Kakonko kwa mwaka 2023.
Washtakiwa hao kwa nia ovu, walighushi saini za Wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Kakonko, Viongozi wa chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kakonko na wajumbe kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, kuonesha kuwa walishiriki maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji yaliyofanyika Machi, 2023 na kulipwa posho za ushiriki wakati si kweli.
Washtakiwa hao walikana mashtaka yote waliyosomewa na walikidhi masharti ya dhamana hivyo wako nje kwa dhamana hadi Julai 29,2025 shauri litakapoitwa tena