NA MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa uchaguzi kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na za kuaminika kwa umma, ili kuepusha taharuki na mkanganyiko katika maeneo wanayoyasimamia, hasa wakati huu wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wito huo umetolewa leo,Julai 17,2025 na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Dk. Zakia Mohamed Abubakar, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa watendaji 119 wa uchaguzi kutoka mikoa ya Tanga na Kilimanjaro yaliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Dk. Abubakar amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika utoaji wa taarifa, akiwataka watendaji kupima na kuthibitisha taarifa kabla ya kuzitoa hadharani ili kuepusha kusambaa kwa habari zisizo sahihi na kuchangia utulivu katika maeneo yao.
“Pima taarifa yako kabla hujaitoa, ili kuzuia taharuki na kuchangia utulivu katika maeneo yenu,” alisema.
Mafunzo haya, yaliyofanyika kuanzia Julai 15 hadi 17, 2025, yalilenga kuwaimarisha watendaji hao katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kwa mujibu wa sheria na miongozo ya uchaguzi.
Amefafanua kuwa utoaji wa taarifa kwa vyombo vya habari ni jukumu muhimu la watendaji wa uchaguzi, hivyo ni lazima taarifa hizo ziandaliwe kwa kina, na ziwe za kweli ili kuepusha mkanganyiko au hofu isiyo ya lazima kwa wananchi.
Aidha, amewakumbusha washiriki wa mafunzo kuhusu kiapo cha kutunza siri walichokula tarehe 15 Julai, akisisitiza kuwa ukiukwaji wa kiapo hicho ni kosa la kisheria linaloweza kuwalazimu kuwajibika kwa mujibu wa sheria.
Pia amewapongeza washiriki hao kwa ukomavu, usikivu na mchango wao wa mijadala, na kuonyesha imani kuwa wamejipanga vyema kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria mpya za Uchaguzi zilizopitishwa mwaka 2024: Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2.
“Katika mafunzo haya mmepata uelewa wa masuala mapya kama usimamizi wa kura za magerezani, jinsi ya kushughulikia kura za Rais kwa wapiga kura walioko nje ya vituo walivyojiandikisha, pamoja na hatua za kuchukua iwapo mgombea mmoja tu atajitokeza wakati wa kampeni,” alifafanua.
Amewasihi washiriki kuwafundisha kwa weledi wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata, pamoja na kusimamia ratiba za kampeni, shughuli za uteuzi na vikao vya vyama vya siasa kwa kuzingatia sheria na miongozo.
Kuhusu matumizi ya vifaa na taarifa za wapiga kura, aliwataka watendaji kuhakikisha mabango, matangazo, na orodha za wapiga kura vinabandikwa kwa wakati kama ilivyoainishwa katika kalenda ya uchaguzi, ili kuepuka malalamiko ya ukiukaji wa sheria.
Aidha, aliwatahadharisha kuhakikisha taasisi na asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura au kuangalia uchaguzi zina vibali halali na zimesajiliwa katika maeneo yao kulingana na orodha rasmi kutoka Tume.
“Kazi za waangalizi ni kutazama uchaguzi tu, si kuingilia au kuhudhuria maeneo ambayo hawajaruhusiwa kufika,” amesisitiza.
Kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu inasema: ‘Kura yako, haki yako jitokeze kupiga kura’.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025 ambapo wananchi watapiga kura kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani.