NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
ASKOFU wa Kanisa la Arise & Shine, Boniphace Mwamposa ‘Bulldozer’amesema ni heshima kubwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jengo jipya la kanisa hilo uliofanyika Kawe, Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo uliofanyika leo Jumamosi Julai 5,2025, Askofu Mwamposa amesema uwepo wa Rais Samia katika tukio hilo ni jambo la baraka na linaonesha wazi kuwa yupo pamoja na wananchi na viongozi wa dini.
Amesisitiza kuwa uwepo wa Rais Samia unaonesha pia ni jinsi gani viongozi wa kitaifa wanathamini mchango wa taasisi za dini katika kujenga maadili na mshikamano wa jamii.
Amesema ujenzi wa Kanisa hilo ulikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu na leo Mungu amemtimizia, na si tu kwa kumalizika kwa jengo hilo, bali pia kwa kulizindua mbele ya Rais wa nchi.
“Hii ni neema ya kipekee, na tulisema ni uzinduzi mkubwa ambao utakwenda mara mbili kwa maana kwamba maisha ya watu kiuchumi, kimaisha na kiafya yatazinduliwa upya, maono yanapofanyika na kuonekana tunamtukuza Mungu,” amesema Mwamposa.
Kanisa hilo jipya limezinduliwa rasmi kwa kufunuliwa jiwe la msingi na Rais Samia, mbele ya maelfu ya waumini, viongozi wa dini, siasa na serikali waliohudhuria ibada hiyo maalumu.