_▪️Asema Serikali itaendelea kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa haki na ustawi wa wafanyakazi
_▪️Atoa wito kwa waajiri kuzingatia matakwa ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi
_▪️Aitaka WCF iendelee kushirikiana na wadau katika sekta ya ajira
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa huduma za fidia kwa wafanyakazi si suala la hiari bali ni haki ya msingi ya mfanyakazi, inayopaswa kulindwa, kuendelezwa na kusimamiwa kwa weledi na uwajibikaji wa hali ya juu.
Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuhakikisha kuwa maendeleo ya nchi yanakwenda sambamba na ulinzi wa haki na ustawi wa wafanyakazi wake.
Amesema hayo leo (Ijumaa, Julai 05, 2025) alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa maadhimisho ya miaka kumi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Waajiri, wafanyakazi na Serikali tunapaswa kuendelea kushirikiana kwa dhati katika kuhakikisha kuwa kazi inaendelea kwa tija, na wakati huo huo, wafanyakazi wanalindwa dhidi ya madhila yanayotokana na kazi wanazozifanya kila siku.”
Aidha, Majaliwa ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wanazingatia kikamilifu matakwa ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kujisajili katika Mfuko, kuwasilisha michango kwa wakati, na kutoa taarifa mapema pale wafanyakazi wanapopata madhila yanayotokana na kazi.
” Kutotimiza wajibu huu ni kutotendea haki ustawi wa wafanyakazi na kulemaza ufanisi wa Mfuko.”
Kadhalika,Majaliwa amesema kuwa Rais Dk. Samia wakati wote ametoa miongozo ya kuhakikisha Serikali inaboresha maslahi ya watumishi wa umma,kuboresha mazingira yakufanyia kazi na Utumishi wa umma kuendeshwa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Waziri wa Nchi- Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa katika jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuboresha ustawi wa Wafanyakazi walioumia kazini, Serikali imekwishatangaza kwenye Gazeti la Serikali Ongezeko la malipo ya fidia ya kila mwezi kwa wanufaika wa Mfuko wa WCF kwa kati ya asilimia 3 hadi asilimia 31 kutegemea mnufaika alistahili kulipwa kuanzia lini.
Ameongeza kuwa WCF imeishi falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo utendaji mzuri wa mfuko huo umeleta mageuzi chanya ya kiuchumi kwa wafanyakazi na kuleta maelewano kati ya wafanyakazi na waajiri ambapo kwa kiasi kikubwa hii imewajengea ari ya kufanya kazi kwa bidii na kuongeza uzalishaji hasa tunapoendelea kujenga uchumi wa viwanda”.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk. John Mduma ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kupunguza kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia moja wakati Mfuko unaanzishwa hadi asilimia sifuri nukta tano (0.5%) hivi sasa. Hiki kilikuwa ni kilio cha waajiri cha muda mrefu
“Tunaipongeza Serikali pia kwa kuwezesha kupunguza kiwango cha riba ya ucheleweshaji wa michango kwa waajiri kutoka asilimia kumi hadi asilimia mbili kwa mwezi. Hatua hii imeongeza imani ya wawekezaji kwa WCF na Serikali kwa ujumla”.
Naye Mwakilishi mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Kazi (ILO) Caroline Mugalla amesema kuwa katika maadhimisho ya miaka 10 ya WCF, jamii inapaswa kukumbuka kuwa kinga ya jamii sio matumizi yasiyo na tija bali ni uwekezaji katika haki, uzalishaji wenye tija unaolifanya Taifa kuwa thabiti. “Tuendelee kujenga Tanzania ambayo kila mfanyakazi anapata huduma stahiki”
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba-Doran amesema kuwa Chama hicho kwa kushirikiana na WCF wamekuwa wakitoa mafunzo na kuhamasisha waajiri kuhusu fidia kwa wafanyakazi.
“Mafunzo haya yameongeza uelewa na kuchangia kupunguza ajali na magonjwa au vifo vinavyotokana nakazi. Tangu mwaka 2016-2024, ATE kwa kushirikiana na WCF tumefanikiwa kutoa mafunzo mara 21 katika Maudhui Kuhusu Sheria ya Fidia kwa Wafanyakaziya mwaka 2008 na kanuni zake, Fidia Mahali pa Kazi, Ajali na Magonjwa.“
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA Rehema Ludanga ameipongeza WCF kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya teknolojia ya habari na Mawasiliano ambayo imeweza kuongeza ufanisi na kuhudumia wanachama wake.
“Tunaipongeza sana Serikali kwa kuendelea kuipa nguvu WCF sisi TUCTA tunaahidi kuendelea kushiriana nao ili mafanikio yazidi kwenda mbele na tunaipongeza kwa kufikia miaka 10 ya faida”
Katika hafla hiyo Majaliwa alizindua fao la utengamao ambalo litamuwezesha mfanyakazi aliyepata madhara kazini kurejeshwa ofisini na kupatiwa kazi mbadala inayoendana na hali yake.