*ASISITIZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI AJENDA YA DUNIA
*ASEMA WIZARA INAITEKELEZA KWA VITENDO
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
NAIBU katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati Jadidifu, Dk.Khatibu Kazungu leo Julai 04, 2025 amepokea magari mawili yatakayotumika kwa ajili ya kampeni ya kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia chini ya kampeni ya nishati safi ya kupikia Okoa Maisha na Mazingira itakayofanyika nchi nzima na Wizara ya nishati kwa kushirikiana na UNCDF.
‘’ Ajenda ya Nishati safi ya kupikia ni ajenda ya Dunia na sisi Wizara ya Nishati tuko tayari kwa utekelezaji ili kumuunga mkono Rais Samia’’ amesema Dk. Kazungu
Aidha, ameishukuru Umoja wa Ulaya, na UNCDF kwa kutekeleza mradi wa nishati safi ya kupikia chini ya mfuko wa Cook fund kwa kuwa umesaidia kubadili maisha na mitazamo ya wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya Nishati safi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Christine Grau amesema umoja wa Ulaya uko tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kwenye utekelezaji wa Nishati safi ya kupikia na tayari EU imetoa kiasi cha Euro Milioni 19.4 sawa na Sh.Bilioni 59 kutekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia kwa mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Pwani, Morogoro na Mwanza.
Kuhusu magari amesema magari hayo mawili yana thamani ya Euro 130,000 na amewataka wizara ya Nishati kuhakikisha wananchi wa vijijini wanafikiwa na nishati safi ya kupikia
Tanzania inajipanga kutekeleza kwa vitendo mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia chini ya mkakati wa Mawasiliano wa Taifa ili kutoa elimu kwa wananchi na kufikia lengo la Serikali la asilimia 80 ya watanzania kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.