NA MWANDISHI WETU, HANDENI, TANGA
WAKULIMA wa Mkonge zaidi ya 5,000 mkoani Tanga, watanufaika kwa kupata uhakika wa soko la mazao yao na bei bora hatua inayotarajiwa kuinua hali yao ya kiuchumi kupitia Mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kuchakata Mkonge unaotekelezwa na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), katika Kijiji cha Taula Wilaya ya Handeni mkoani hapa.
Aidha mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh Milioni 710, pia utazalisha ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi wapatao 150 huku wafanyabiashara wadogo na wa kati wakifanikiwa kupanua biashara zao kwa kutoa huduma mbalimbali kwa kiwanda na wafanyakazi wake, hivyo kuchochea ukuaji wa biashara katika eneo hilo.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TSB, Profesa Esther Dungumaro wakati wajumbe wa bodi hiyo walipotembelea mradi huo na kujionea ujenzi unaoendelea sanjari na kutembelea Shamba la Mkonge la Kibaranga wilayani Muheza ambalo linaendelea na maboresho ya miundombinu ya uchakataji Mkonge na Shamba la Ufugaji la Mruazi.
Prof. Dungumaro amesema maboresho hayo yanaendelea katika sehemu mbalimbali yakianzia mkoani Tanga.
“Handeni ni eneo mojawapo ambalo tunajenga kiwanda cha kuchakata Mkonge. Ikumbukwe Serikali ya Awamu ya Sita imehamasisha sana wakulima wa zao la Mkonge miaka mingi iliyopita zao hili lilikuwa linaibeba nchi yetu kitaifa na kimataifa.
“Kwa sasa kwa busara za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan umefanyika uhamasishaji kwa wakulima wa Mkonge lakini changamoto ambayo tunakutana nayo ni viwanda vichache vya uchakataji hivyo Rais alitoa agizo viwanda vijengwe ili kuwasaidia wakulima wadogo kuchakata Mkonge wao.
“Kwa hiyo sisi kama bodi tukishirikiana na Menejimenti ya TSB na Waziri wa Kilimo, tumeanza kutekeleza ujenzi wa viwanda vya kuchakata Mkonge tukianzia hapa Handeni lakini tutakwenda, Lushoto, Korogwe na Mkinga,” amesema.
Amesema hatua hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais kwamba miundombinu iboreshwe na wakulima wadogo wapate fursa ya kuchakata mkonge wao.
“Kwa hiyo kama Makamu Mwenyekiti, napenda kumpongeza Rais na kumueleza kuwa tumetekeleza maagizo yake kwa vitendo na tunakoelekea tutahakikisha kwamba changamoto za mitambo na viwanda vya uchakataji Mkonge vinakwenda kuisha na viwanda vingine vitajengwa katika mikoa mingine,” amesema.
Akizungumzia shamba la Kibaranga amesema kwa wanaofahamu Tasnia ya Mkonge, shamba hilo lina mchango mkubwa sana kinachofanyika hivi sasa ni maboresho ya eneo hilo na ukarabati wa mashine ya kuchakata Mkonge.
“Tunaishukuru serikali si tu kwamba wakulima wadogo watafaidika kuhakikisha Mkonge wao hauharibiki unachakatwa kwa wakati lakini pia itaongeza ajira ambalo ni jambo jema.
Naye Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa wa Kijiji cha Taula, Zaina Mohamed amesema Mradi wa ujenzi wa Kiwanda hicho ni mkombozi wa kijiji hicho kwani licha ya wakulima kufaidika lakini vijana wa kijiji hicho na maeneo jirani wamefaidika na ajira.
“Nikiwa kama mwenyekiti nimepambana kuhakikisha na sisi hapa tunakuwa na uwezo wa kusema nakwenda kazini kwa sababu awali tulikuwa tunakwenda kufanya kazi katika vijiji vingine na watoto wetu walikuwa wakimaliza shule wanakwenda kutafuta ajira Dar es Salaam lakini kwa mradi huu watatulia hapa kijijini.
“Tunamuomba rais kama kuna mradi mwingine Taula tuko tayari tuna maeneo ya kutosha,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti Chama cha Ushirika cha Kibaranga (Kibaranga Amcos), Paulo Haule amesema kwa ukarabati unaoendelea licha ya ajira lakini utawaingizia kipato kwani wakulima wa Muheza na majirani zetu ambao ni Wilaya ya Mkinga watapata fursa ya kupeleka Mkonge wao badala ya kupeleka maeneo mengine.
“Tunamshukuru Rais kwa kutuwezesha sisi wakulima wadogo kupata viwanda kama hivi na kukarabati kiwanda chetu ili hatimaye wananchi waweze kuboresha maisha yao,” amesema.