*MAJALIWA ,MKENDA NA D.C MTAMBULE WAIPONGEZA TET
*KAULI MBIU YA MWANAFUNZI MMOJA KITABU KIMOJA YAFIKA MAHALA PAKE
*MTAMBULE ASEMA KINONDONI HAKUNA UPUNGUFU WA VITABU WALA MADARASA
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk.Aneth Komba amesema maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi yake ni Jubilei ya dhahabu kutokana na mafanikio ya kielimu yaliyopatikana
Dk.Komba amesema kuwa katika kipindi cha miaka 50, Serikali kupitia TET imefanikiwa kuongeza hazina ya vitabu vya ziada, rejea, Riwaya, Hadithi, ushairi na aina nyingine ya uandishi bunifu pamoja na moduli na maudhui ya kielektroniki yanayolenga kuwaongezea maarifa wanafunzi kwa kutathmini vitabu vya ziada aina 1446 vinavyoandikwa na wachapishaji binafsi
Vile vile Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh. Bilioni 2.6 kati ya Sh. Bilioni 4.3 zilizoahidiwa na wadau mbalimbali kupitia kampeni ya Kitabu Kimoja, Mwanafunzi Mmoja.
Haya yamebainishwa leo Jumanne Juni 17,2025 katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya TET yaliyofanyika jijini Dar es salaam .
Aidha Dk. Komba amesema katika miaka 50 ijayo TET itaendelea kujiimarisha na kuwa kitovu maridhawa cha ubora katika uandaaji, ukuzaji na ubunifu wa mitaala sambamba na Kuimarisha tafiti ili kuiwezesha serikali kuendelea kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusiana na utoaji wa elimu katika ngazi ya Elimumsingi kwa kuzingatia matokeo ya tafiti.
Amesema TET itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia mpya na mbinu za kisasa za ufundishaji na ujifunzaji zinazotangamanisha matumizi ya zana za kidijiti na akili unde na Kuimarisha viwanda vya uchapaji kwa kuboresha miundombinu na kununua machine za kisasa kwani mashine zilizopo sasa zinatumia teknolojia ambayo imepitwa na wakati.
Katika hili, Dk.Komba amejinasibu kuwa TET imeazimia kujenga kiwanda kikubwa cha uchapaji ili kupunguza gharama, kuongeza ajira, kuongeza mapato ya Taasisi na kuharakisha upatikanaji wa machapisho.
” Kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya TET na taasisi na mashirika ya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuendelea kuweka mazingira rafiki katika uboreshaji wa elimu nchini pamoja na kujifunza kutoka kwa nchi nyingine. ” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo.
Wakati huo huo Dk.Komba amesema
TET inatambua na kuthamini sana mchango wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan hususani katika kazi ya uandishi, uchapaji na usambazaji wa vitabu.
“Taasisi imeona umuhimu wa kuunga mkono juhudi hizi za Mheshimiwa Rais kwa kushirikisha wadau katika kusaidia jitihada za Serikali kufika lengo la kila mtoto kupata kitabu kimoja.
Kauli hiyo inakwenda sambamba na malengo ya mipango ya miaka 50 ijayo ikiwemo mwendelezo wa uboreshaji elimu na ujenzi wa kiwanda kikubwa na cha kisasa cha uchapaji kinachotarajiwa kupunguza na kuokoa gharama za uchapaji hasa wa vitabu.
” Hivyo basi Kauli mbiu ya maadhimisho yetu ya miaka 50 ni “Kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja, Mpekitabu gusa ndoto”. Kauli hii inalenga kuboresha uwiano wa vitabu kwa wanafunzi kutoka kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu (1:3) kuwa kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja (1:1) kwa kila somo. “ameeleza Dk.Komba
Aidha, Dk. Komba ameongeza kuwa kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na sita kauli mbiu hii inalenga kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwa kutoa Kompyuta Mpakato Moja kwa mwanafunzi mmoja kwa mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho hayo amesema kuwa Serikali itaendelea kuiimarisha Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ili ifikie maono ya kuwa kitovu maridhawa cha ubora katika uandaaji, ukuzaji na ubunifu wa mitaala.
Ameeleza kuwa TET ni moyo wa ukuaji wa elimu nchini na hasa kwa kuwa ndiyo inayojenga msingi wa elimu kuanzia Darasa la Awali hadi Kidato cha Sita.
“Serikali inatambua wakuza mitaala wanafanya kazi kwa bidii, weledi, maarifa na moyo wa kizalendo sana. Hivyo, niwahakikishia Watanzania wote kuwa, wakati wote Serikali, itaendelea kuimarisha utendaji wa TET ili kwenda sambamba na kazi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia.”
Pamoja na mambo mengine,Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iimarishe ushirikiano na taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi ili TET ipate uzoefu zaidi katika kuandaa mitaala, kuandaa vifaa vya mtaala na kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini.
“Hii ina maana ya kuwepo kwa ziara za ndani na nje ya nchi kwenda kupata uzoefu, msijifungie hapa tu, nendeni mkaone wenzenu wanafanya nini, ili muendelee kufanya maboresho zaidi kwenye taasisi yenu”
Amesema kuwa mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika masuala ya uandaaji wa mitaala, vitabu vya kiada na vifaa vingine vya utekelezaji wa mitaala, matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyingine katika utoaji wa huduma zenu pamoja na utoaji wa mafunzo kwa walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala.
Pia Majaliwa ameipongeza taasisi hiyo kwa mapinduzi makubwa ya matumizi ya TEHAMA na mifumo wa kidijitali. Katika hili nimejionea mwenyewe katika maonesho yenu kuwa hata walimu wenye mahitaji maalumu wanaweza kutumia maktaba mtandao na mfumo wa kidijitali haya ni mapinduzi makubwa katika kipindi hiki cha miaka 50”
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amempongeza Rais Dk Samia kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu nchini
“Ni kazi kubwa sana imefanyika katika kuandaa mitaala mipya, wakati Serikali ilipokuwa inazindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023 tulikuwa tunatekeleza maono yake”
Waziri Mkenda pia ameipongeza TET kwa kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1975 kwa kusema kwamba inafanya vizuri .
” Ninapenda kuipongeza TET kwa
shindano la tuzo za Uandishi bunifu sambamba na Tuzo za Ufundishaji kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari.” amesisitiza Mkenda
Naye Mkuu wa Wilaya Saad Mtambule ameipongeza TET kwa maadhimisho ya miaka 50 na kusisitiza kuwa Kwa Wilaya yake ya Kinondoni Elimu imeendelea kuimarika katika suala zima la upatikanaji vitabu na madarasa ya kutosha.
“Katika Wilaya ya Kinondoni hatuna shida ya vitabu wala Madarasa hizi ni juhudi za Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Wizara pamoja na Wadau mbalimbali wa Elimu ikiwemo TET” amehitimisha Mtambule kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.
Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya TET yalipambwa na burudani mbali mbali ikiwemo Kwaya,Mashairi na nyimbo .